2017-02-24 14:37:00

Maji ni sehemu ya haki msingi za binadamu!


Maji ni sehemu ya haki msingi za binadamu na inaendelea kuwa ni changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa. Ikiwa kama suala zima la maji halitashughulikiwa kikamilifu, kwa siku za usoni, linaweza kuwa ni chanzo kikuu cha kinzani na migogoro ya kimataifa. Maji safi na salama ni muhimu sana katika mchakato mzima wa maboresho ya afya ya binadamu.

Kutokana na changamoto ya maji duniani, Taasisi ya Kipapa ya Sayansi, kwa muda wa siku mbili, kuanzia tarehe 23- 24 Februari 2017, imekuwa ikifanya semina ya kimataifa kuhusu haki ya maji kwa kuwashirikisha wataalam 96 kutoka katika sekta ya maji na afya, sehemu mbali mbali za dunia, ili kuchambua maji kama sehemu ya haki msingi za binadamu. Lengo kama anavyo kaza kusema Baba Mtakatifu Francisko ni kujenga utamaduni na madaraja ya watu kukutana, ili kujadiliana  katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Semina hii inawashirikisha “vigogo” wa dunia katika sekta ya maji safi na salama inayosimamiwa na kuratibiwa na Askofu Marcelo Sànchez Sorondo, Mkuu wa Taasisi ya Kipapa ya Sayansi. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote ameonesha umuhimu wa kulinda, kutunza na kudumisha mazingira kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hapa kuna haja ya kusimama kidete kuwa na sera zitakazosimamia na kuendeleza ekolojia katika ukamilifu wake. Maji ni chanzo kikuu cha uhai wa binadamu.

Kumbe, uhaba wa maji safi na salama unaweza kuwa ni chanzo cha migogoro na kinzani kwa siku za usoni, ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa haitasimama kidete kulinda vyanzo vya maji pamoja na kutambua kwamba, maji ni sehemu ya haki msingi za binadamu. Kumbe, huduma bora za maji safi na salama ni kichocheo kikuu cha maisha na afya bora zaidi. Takwimu za Shirika la Afya Duniani kwa Mwaka 2014 zinaonesha kwamba, zaidi ya watu milioni 748 hawakuwa na uwezekano wa kupata huduma ya maji safi na salama; hali inayogumisha maisha ya wanawake na wasichana wengi duniani wanaopaswa kusafiri umbali mrefu ili kutafuta maji kwa matumizi ya binadamu, hali inayopunguza tija na uzalishaji.

Lakini ikumbukwe kwamba, dhana ya maji kuwa ni sehemu ya haki msingi za binadamu ni agenda iliyoibuliwa hivi karibuni, lakini inaendelea kushika kasi kubwa sana katika Jumuiya ya Kimataifa kutokana na unyeti wake! Ndiyo maana kuna haja ya kuwa na miundo mbinu ya kisheria, kiufundi, kijamii na kisiasa ili kuanzisha mchakato wa ujenzi wa “utamaduni wa utunzaji bora wa maji”. Kwa njia hii, amani duniani inaweza kuimarishwa kwa kuzuia vita, kinzani na migogoro inayoweza kufumbatwa katika mafao ya kisiasa na kiuchumi kwa kubeza utu na maisha ya binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.