2017-02-23 12:07:00

Padre Lombardi, SJ., atunukiwa tuzo ya heshima na Rais wa Ufaransa


Padre Federico Lombardi, Rais wa Mfuko wa Joseph Ratzinger amemshukuru Rais wa Ufaransa kwa kutambua mchango wake katika kazi na dhamana aliyokuwa amekabidhiwa na Kanisa. Anatambua uhusiano wake na Ufaransa tangu bado akiwa ni kijana, kama mzaliwa wa Torino, Kaskazini mwa Italia; mwanachama wa Skauti aliyebahatika kuvuka milima na mabonde hadi kuingia nchini Ufaransa, lakini zaidi, alipenda na kujisikia vizuri sana alipokuwa anashiriki huduma kwa wagonjwa kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Lourdes.

Kama Myesuit anajisikia kuwa na mahusiano ya pekee na Ufaransa ambayo anaiona kuwa ni nchi yake ya pili kutokana na historia ya maisha na wito wake. Padre Lombardi ameyasema haya Jumatano jioni, tarehe 22 Februari 2016 kwenye Ubalozi wa Ufaransa mjini Vatican, alipokuwa anapokea tuzo ya heshima kutoka kwa Rais wa Ufaransa.

Padre Lombardi anasema, katika maisha yake alibahatika kufanya kazi karibu sana na Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na taasisi mbali mbali za Vatican na katika mazingira kama haya aliweza pia kuwahudumia wananchi, historia na utamaduni wa wananchi wa Ufaransa. Amekubali kwa moyo wa furaha na shukrani kupokea tuzo hii kwa niaba ya watu na taasisi zote zilizomwezesha kutoa mchango wake na kwa namna ya pekee Radio Vatican ambayo kwake iligeuka kuwa ni nyumba yake ya pili; alijisadaka bila ya kujibakiza ili kuhakikisha kwamba, wananchi wa Ufaransa na wajuani wao wanafaidika na huduma iliyokuwa inatolewa na Radio Vatican.

Hii ni huduma ya matumaini, furaha na mahangaiko ya Kanisa la Kiulimwengu. Hapa wameshiriki wadau mbali mbali katika tasnia ya habari; vituo vya Radio vilivyokuwa vinatumia lugha ya Kifaransa kurusha tena matangazo ya Radio Vatican sehemu mbali mbali za dunia kwa kutumia Masafa Mafupi; baadaye matangazo yakaanza kurushwa kwa njia ya Satelite na sasa Radio Vatican inaendelea kutambaa katika mitandao ya kijamii. Ni matumaini ya Padre Lombardi kwamba, huduma hii itaendelezwa na kukuzwa kwa kusoma alama za nyakati.

Padre Lombardi anasema, alipokuwa Msemaji mkuu wa Vatican na Mkurugenzi wa Kituo cha Televisheni cha Vatican, alibahatika kushirikiana na wadau mbali mbali waliokuwa “wanaimanya” vyema lugha ya Kifaransa; wakati wa matangazo ya kawaida, nyakati za ziara za kichungaji za Baba Mtakatifu. Anawashukuru wote hawa kwa urafiki na ushirikiano waliomwonesha na kumshikirisha kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo. Mwishoni, anasema, ataendelea kuwa ni rafiki mwaminifu wa nchi ya Ufaransa, watu na utamaduni wake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.