2017-02-23 13:49:00

Jumuiya ya Kimataifa inakuna kichwa kuhusu baa la njaa duniani!


Taarifa ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO kwa Mwaka 2017 inasema, lengo la Jumuiya ya Kimataifa kufuta baa la njaa duniani ifikapo mwaka 2030 pengine lisifikiwe kutokana na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza kwa sasa duniani. Kumekuwepo na matumizi makubwa ya rasilimali za dunia kupita kiasi; athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na ukosefu wa usawa kati ya watu. Mbinu mkakati wa uhakika wa usalama wa chakula duniani ulishafikiwa takribani miaka thelathini iliyopita, lakini athari za mabadiliko ya tabianchi ni kati ya mambo mapya yanayotishia usalama wa maisha ya watu wengi duniani. Kumekuwepo na ukatati mkubwa wa misitu kwa matumizi ya binadamu, hali ambayo imesababisha kukaukwa kwa vyanzo vya maji sehemu mbali mbali za dunia na hivyo kupelekea ukame unaoendelea kutishia usalama na maisha ya mamilioni ya watu duniani.

Kama huu ndio utakaokuwa mwelekeo kwa Jumuiya ya Kimataifa, kuna hatari kubwa kwa siku za usoni kuweza kuwa na uhakika wa usalama wa chakula anasema Prof.  Josè Graziano da Silva, Mkurugenzi mkuu wa FAO. Ifikapo mwaka 2050 idadi ya watu duniani inakadiriwa kufikia billioni 10 na hivyo, kutakuwepo na uhitaji mkubwa wa chakula kwa walau asilimia 50% ya hali ya sasa, kiasi hata cha kuathiri mfumo wa maisha na chakula katika ujumla wake. Kutakuwepo na ukataji mkubwa wa miti kwa ajili ya matumizi ya binadamu; uharibifu wa mazingira pamoja na uzalishaji mkubwa wa gesi ya ukaa. Mabadiliko ya tabianchi yatakuwa na athari kubwa sana katika sekta ya kilimo kutokana na mafuriko pamoja na ukame wa kutisha.

FAO inasema, dunia ina uwezo wa kuzalisha chakula cha kutosha kwa wote, lakini jambo la msingi ni watu kubadili tabia na mfumo wa maisha. Changamoto mamboleo zinaonesha kwamba, itakuwa ni muujiza kwa Jumuiya ya Kimataifa kutokuwa na njaa ifikapo mwaka 2030. Kumbe, hapa kuna haja ya kufanya mageuzi makubwa katika mfumo mzima wa kilimo; kwa kuwajengea wakulima vijijini uwezo wa kiuchumi sanjari na udhibiti na matumizi bora zaidi ya rasilimali za dunia; kama sehemu ya maboresho ya afya kwa watu wengi zaidi.

Kilimo kitapaswa kuboreshwa maradufu na watu kujenga utamaduni wa kupanda na kutunza miti. Lazima kuwepo na sera makini za kilimo bora na cha kisasa; utunzaji wa vyanzo vya maji pamoja na udhibiti wa uzalishaji wa hewa ya ukaa. Wakulima wadogo wadogo vijijini wawezeshwe kikamilifu, ili kuwa na uhakika wa usalama wa chakula kwa watu wengi zaidi sanjari na kupambana utapiamlo mkali. Watu tangu wakati huu wajifunze kuwa na matumizi bora zaidi ya ardhi, vyanzo vya maji pamoja na kujikita katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Ili kufikia lengo, hili kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa katika ngazi mbali mbali kuwekeza katika sekta ya kilimo, mifugo na misitu; kuhamasisha tafiti zitakazoisaidia Jumuiya ya Kimataifa kupambana na ukosefu wa maji safi na salama kwa matumizi ya binadamu pamoja na udhibiti wa athari za mabadiliko ya tabianchi. Kuwepo na mshikamano wa dhati miongoni mwa wakulima, usambazaji na ugavi wa mazao ya kilimo pamoja na kuwa na sera makini katika kupanga bei ya mazao ya kilimo pamoja na usimamizi makini wa uzalishaji katika sekta ya kilimo.

Taarifa ya FAO inaonesha kwamba, kumekuwepo na mwelekeo wa ongezeko la idadi ya watu hasa mijini sanjari na ongezeko la umri wa; mabadiliko ya tabianchi, matumizi makubwa ya rasilimali ya dunia; mahitaji makubwa ya mazao ya kilimo; mlipuko wa magonjwa; vita, kinzani na mipasuko ya kijamii; usugu wa umaskini, ukosefu wa usawa na ongezeko la majanga asilia. Ukosefu wa lishe bora; mabadiliko ya miundo mbinu na ukosefu wa fursa za ajira; wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji; mabadiliko ya mfumo wa uzalishaji wa chakula na maisha ya wakulima wenyewe; uharibifu na upotevu wa chakula; mabadiliko katika mifumo ya ufadhili wa miradi ya maendeleo kimataifa; uhakika na usalama wa chakula kimataifa.

FAO inakaza kusema, kuna changamoto kubwa kwa sasa ni kuhusuuzalishaji wenye tija katika sekta ya kilimo kutokana naongezeko kubwa la mahitaji ya chakula duniani. Changamoto nyingine ni kuwa na uhakika wa rasilimali asilia; kudhibiti athari za majanga asilia; kung’oa umaskini wa hali na kipato sanjari na maboresho ya usawa kati ya watu. Kufutilia mbali baa la njaa na utapiamlo mkali. Kuboresha mfumo wa chakula kwa kuongeza tija na kuiwezesha kuwa ni shirikishi zaidi. Changamoto nyingine ni maboresho ya uwezo wa kiuchumi kwa wananchi wa vijijini; kupambana na vita, kinzani na migawanyiko ya kijamii; kudhibiti mambo yote yanayohatarisha mfumo wa chakula duniani pamoja na utawala bora.!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S,

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.