2017-02-22 09:17:00

Vigogo wa Mfuko wa Yohane Paulo II kwa Sahel wanakutana Dakar!


Baraza Kuu la Mfuko wa Yohane Paulo II Ukanda wa Sahel, ulioanzishwa kunako mwaka 1984 ili kupambana na kuenea kwa Jangwa na Sahara, limeanza mkutano wake wa mwaka tarehe 21 Februari na unatarajiwa kuhitimishwa tarehe 25 Februari 2017 huko Dakar, Senegal. Mfuko huu kwa sasa unasimamiwa na kuratibiwa na Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu. Katika mkutano huu, Monsinyo Giampietro Dal Toso, Katibu mwakilishi Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu anashiriki kama mtazamaji wa kudumu kutoka Vatican.

Maaskofu wanaoshiriki mkutano huu ni wale wanaotoka Burkina Faso, Senegal Mauritania, Niger, Cape Verde, Ciad, Gambia, Guinea Bissau na Mali, wanaongozwa na Askofu Sanou Lucas Kalfa kutoka Burkina Faso ambaye kwa sasa ndiye Mwenyekiti. Ujumbe kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Italia na Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani unashiriki kwani, wao ndio wafadhili wakuu wa Mfuko wa Yohane Paulo II kwa Ukanda wa Sahel. Miradi inayopembuliwa na kujadiliwa kwa mwaka 2016 ilikuwa ni 43 kutoka katika nchi 6 iliyo gharimu kiasi cha Dola za Kimarekani 550, 000. Hadi kufikia mwaka 2015 jumla ya miradi 3, 200 ilipitishwa na kugharimiwa kwa kiasi cha Dola za Kimarekani zaidi ya milioni 37.

Miradi inayotekelezwa kwa niaba ya Khalifa wa Mtakatifu Petro ni ile ya kupambana na Jangwa la Sahara, ili kuweza kuboresha mazingira, nyumba ya wote kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko. Ni miradi inayopania kuinua ubora na tija katika sekta ya kilimo ili kuweza kuwa na uhakika wa usalama wa chakula; maji safi na salama kwa ajili ya matumizi ya binadamu. Mfuko huu unafadhili pia miradi ya teknolojia rafiki kwa ajili ya nchi wanachama wa Mfuko wa Yohane Paulo II kwa Ukanda wa Sahel.

Tangu kuanzishwa kwake, Mfuko huu umekuwa na manufaa makubwa kwa wananchi wa Sahel kwani umesaidia mafunzo kwa wataalam; mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene katika huduma, kwani sehemu kubwa ya watu wanaofaidika na mradi huu ni waamini wa dini ya Kiislam. Hali ngumu ya maisha inayoendelea kuwatumbukiza watu wengi katika umaskini inasababishwa kwa kiasi kikubwa na vita, ukame na baa la njaa na utapiamlo pamoja na misimamo mikali ya kidini na kiimani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.