2017-02-21 08:14:00

Papa Francisko Jimboni Genova anataka kuwaimarisha ndugu zake!


Baba Mtakatifu Francisko tarehe 27 Mei 2017 anatarajiwa kutembelea Jimbo kuu la Genova, Kaskazini mwa Italia, ili kuwaimarisha ndugu zake katika imani kwa Kristo na Kanisa. Hivi ndivyo anavyosema, Kardinali Angelo Bagnasco, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Genova, Italia katika ujumbe kwa familia ya Mungu Jimboni mwake, wakati huu wanapoendelea kufanya maandalizi, hasa ya maisha ya kiroho, ili kumpokea na kumkarimu Baba Mtakatifu Francisko atakapowatembelea. Hiki ni kipindi cha sala, toba na wongofu wa ndani, unaopania kuwasaidia waamini kweli kufaidika na hija ya Baba Mtakatifu Francisko Jimboni mwao.

Waamini wanakumbushwa kwamba, kunako mwaka 1985, Mtakatifu Yohane Paulo II alitembelea Jimboni humo kwa mara ya kwanza katika historia na kurejea tena Jimboni humo kunako mwaka 1990. Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI akatembelea Jimbo kuu la Genova, kunako mwaka 2008 na hapo akaacha chapa ya kudumu katika sakafu ya mioyo ya watu wa familia ya Mungu Jimboni Genova. Kwa sasa hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko miongoni mwao inapania pamoja na mambo mengine anasema, Kardinali Bagnasco ni kuwaimarisha waamini katika imani yao kwa Kristo na Kanisa lake; tayari kuzindua mpango mkakati wa ari na moyo wa kimissionari, unaoamsha na kupyaisha nguvu ya huduma kwa ajili ya mafao ya wengi; kuwaimarisha wale waliokata na kukataatishwa tamaa kutokana na changamoto mbali mbali za maisha.

Ni hija inayopania kuwafariji wazee na wagonjwa pamoja na kuwatia shime vijana wa kizazi kipya kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu ili kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Wakati wote huu wa maandalizi, Jimbo kuu la Genova linapokea sadaka itakayowasilishwa kwa Baba Mtakatifu kama sehemu ya mchango wao kwa huduma ya upendo inayotekelezwa na Baba Mtakatifu sehemu mbali mbali za dunia. Kiini cha hija hii ya kichungaji ni Ibada ya Misa Takatifu, itakayoadhimishwa kwenye eneo la “Fiera del Mare”. Familia ya Mungu kuzunguka Jimbo kuu la Genova inakaribishwa kwa mikono miwili.

Ratiba elekezi ya ziara ya Baba Mtakatifu Francisko Jimbo kuu la Genova inaonesha kwamba, atapata nafasi pia ya kuzungumza na wawakilishi wa waamini wa Jimbo kuu; wafanyakazi; Wakleri, watawa na majandokasisi wanaojiandaa kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake; vijana wa kizazi kipya wanaoendelea kuchakarika usiku na mchana ili kuwashirikisha vijana wenzao ile furaha ya Injili ya Kristo. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu atapata chakula cha mchana na maskini pamoja na wale watu wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii ili kuwaonjesha huruma na upendo wa Baba wa milele ambaye kamwe habagui wala kumtenga mtu awaye yote, kwani wote wameumbwa kwa sura na mfano wake. Atawatembelea na kuwasalimia watoto waliolazwa kwenye Hospitali ya Watoto ya “Giannina Gaslini”.

Kardinali Angelo Bagnasco ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia anakaza kusema, kuanzia tarehe 15- 18 Septemba 2016, Jimbo kuu la Genova lilibahatika kuwa ni mwenyeji wa Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa; tukio ambalo bado wanalikumbuka kwa moyo wa furaha na shukrani. Kumbe, familia ya Mungu Jimbo kuu la Genova inapaswa kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya ujio wa Baba Mtakatifu Francisko Jimboni humo kwa ari na moyo mkuu, ili kweli matukio haya muhimu katika maisha na utume wa Kanisa yaweze kuleta matunda yanayokusudiwa katika maisha ya watu na kwa ajili ya mafao ya wengi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.