2017-02-21 14:19:00

Kipaumbele cha kwanza ni Gabon, mafao ya wengi, haki na amani!


Baraza la Maaskofu Katoliki Gabon linasema, litaendelea kusimama kidete ili kuhakikisha kwamba, linasaidia kuendeleza mchakato wa haki, amani na maridhiano kati ya wananchi wote wa Gabon, daima mafao ya wengi yakipewa kipaumbele cha kwanza, baada ya patashika nguo kuchanika kufuatia mtikisiko wa kisiasa nchini humo baada ya mchakato wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2016 kugomewa na baadhi ya wanasiasa, kwa kutaka kura zihesabiwe upya! Maaskofu Katoliki wanakaza kusema mustakabali wa Gabon na watu wake unapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza na wala si kwa ajili ya baadhi ya viongozi wenye uchu wa mali, fedha na madaraka kwa ajili ya mafao yao binafsi!

Baraza la Maaskofu Katoliki Gabon, hivi karibuni limeitaka familia ya Mungu nchini humo kusimama kidete, kuwa na ujasiri ili kuonesha uzalendo na kamwe isiwe ni bdendera kufuatia upepo! Wananchi wawe imara katika kulinda na kukuza umoja na mshikamano wa kitaifa dhidi ya watu wachache wanaotaka kuwagawa kwa misingi ya ukabila, udini na umajimbo; mambo ambayo hayana tija wala mashiko kwa ustawi na maendeleo ya wananchi wa Gabon.

Maaskofu wanataka vijana kuwa macho na makini na kamwe wasikubali kutumiwa na wanasiasa uchwara kwa ajili ya masilahi yao binafasi, kwani waathirika wakubwa ni vijana wenyewe pale mambo yanapokwenda kombo! Mpasuko wa kisiasa nchini humo, iwe ni changamoto ya kujikita katika mchakato wa haki, amani, maridhiano na umoja wa kitaifa; kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu daima yuko pamoja nao! Wananchi waendelee kufumbata amani, kwani amani ikitoweka mioyoni na akilini mwao, itakuwa ni vigumu sana kuweza kuirejesha tena.

Maaskofu wanasema, hiki ni kipindi tete ambacho kila mwananchi anatakiwa kuwa makini kwa kujizatiti zaidi katika kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho. Pale ambapo kuna kinzani, misigano na mipasuko ya kijamii, wananchi wawe na ujasiri wa kuweka tofauti zao kando, tayari kuanza mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wengi wa Gabon. Uchaguzi mkuu uliofanyika Mwezi Agosti, 2016 umechochea mpasuko zaidi miongoni mwa wananchi wa Gabon.

Majadiliano ya kisiasa yaendelezwe ili yaweze kuwa ni jukwaa la kutafutia ufumbuzi wa changamoto mbali mbali zinazojitokeza nchini humo. Kuna haja ya kuangalia pia kiwango cha kima cha chini cha mshahara ambao kimsingi hautoshelezi mahitaji msingi ya wananchi wengi, kiasi cha kushindwa hata kwa wazazi katika familia kutekeleza dhamana na wajibu wao ndani ya familia. Kuna idadi kubwa ya vijana wasiokuwa na fursa za ajira, hatari sana kwa amani na utulivu wa nchi kwani wanasiasa uchwara wanawatumia vijana hawa kwa ajili ya mafao yao binafsi.

 

Kuna haja ya kuangalia uwezekano pia wa kupunguza kodi zisizo za lazima, ili kuwaondolea wananchi kero! Lakini, pia wananchi wana haki ya kufahamu jinsi kodi yao inavyotumika kama kichocheo cha maendeleo endelevu ya binadamu! Kumbe, wanapaswa kuona matokeo ya fedha inayokusanywa kutoka kwenye kodi na vyanzo vingine vya mapato ya Serikali ya Gabon.

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.