2017-02-17 15:11:00

Vyama vya kiraia na mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi na uchumi


Zaidi ya viongozi 700 wa Jumuiya za Kidini kutoka katika nchi 12 duniani, tangu tarehe 16 hadi 19 Februari 2017 wanafanya mkutano wa kimataifa wa Shirikisho la vyama vya kijamii kimataifa, unaojadili kuhusu ubaguzi wa rangi, uhamiaji, fursa za ajira, makazi sanjari na haki mazingira! Kauli mbiu ya mkutano huu ni “Watu walionja sera za ubaguzi wa rangi na kiuchumi katika ujenzi wa jamii wanashirikisha historia zao na kiu ya mabadiliko”.  Baba Mtakatifu Francisko amewatumia ujumbe washiriki wa mkutano huu wa kimataifa kwa kujikita katika uchambuzi wa masuala nyeti yanayogusa kwa namna ya pekee: ardhi, kazi na makazi!

Baba Mtakatifu anasema, Vatican kwa upande wake, itaendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na vyama vya kijamii kama sehemu ya mchakato wa kubomoa kuta za utengano, utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine; ubaguzi wa rangi na hali ya kutovumiliana. Vyama vya kitaia vinahamasishwa na Baba Mtakatifu kushikamana ili hatimaye, viweze kusimama kidete kubomoa kuta za woga na wasi wasi usiokuwa na mashiko, ili kujenga madaraja ya watu kukutana ili kudumisha upendo. Haya ni mambo ambayo pia yalijadiliwa kwa kina na mapana wakati wa Mkutano wa tatu wa Vyama vya Kiraia uliofanyika hivi karibuni mjini Roma. Kiini cha changamoto zote hizi ni uchu wa fedha, mali na madaraka.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusoma alama za nyakati, ili kujizatiti kikamilifu kupambana na changamoto zinazotaka kudhalilisha utu, heshima na mafao ya wengi. Hatari zilioko mbele yao ni kutowatendea haki jirani zao na kwamba, wao mbele yao kuna fursa ya kuweza kufanya mabadiliko katika maisha ya watu! Wanakumbushwa kwamba, jirani ni mtu yeyote anahitaji msaada wa hali na mali, ili kutenda kwa ari na moyo mkuu kama alivyofanya Msamaria mwema anayesimuliwa kwenye Injili ya Luka 10: 25- 37. Waamini wanapaswa kutenda kwa haki, huruma na mapendo, huku wakijitahidi kumwilisha Amri kuu ya upendo kwa Mungu na jirani.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, uchumi mamboleo unajikita katika rasilimali fedha na faida kubwa, lakini ni uchumi usioguswa na mahangaiko yaw engine na matokeo yake ni kumong’onyoka kwa tunu na kanuni maadili na utu wema. Ukosefu wa fursa za ajira, vita, kinzani na mipasuko ya kijamii inaendelea kushamiri kama uyoga! Demokrasia inawekwa njiapanda, usalama unatoweka na maumbano yanazidi kuongezeka. Hii inatokana na ukweli kwamba, wanasiasa, wachumi na watunga sera hawajaguswa na mahangaiko ya jirani zao, yaani maskini “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi”!

Wakristo wanapaswa kujitambulisha kama Wasamaria wema na Kanisa ndiye mtunza nyumba anayewahudumia wote wanaokimbilia huruma, upendo na tunza yake. Hizi zinapaswa kuwa ni Jumuiya za Kikristo zinazosimiwa katika mshikamano wa upendo ili kuwahudumia watu kiroho na kimwili pasi na unafiki wala bila kuwageuzia kisogo, kuwabagua na kuwatenga, kama sehemu ya mchakato wa kupambana na ukosefu wa haki jamii; kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote pamoja na kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta usalama, hifadhi na maisha bora zaidi.

Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, athari za mabadiliko ya tabia ni kubwa sana, changamoto kwa watu wote kushikamana ili kulinda, kutunza na kudumisha mazingira bora. Ni wakati wa kupinga vitendo vya kigaidi na kamwe dini zisiwe ni chanzo cha kinzani na mipasuko ya kijamii. Biashara haramu na matumizi ya dawa za kulevya inapaswa kudhbitiwa sanjari na kuondokana na misimamo mikali ya kidini na kiimani, ili kujenga misingi ya upendo na amani kama anavyokazia Mtakatifu Francisko katika sala yake anayomwomba Mwenyezi Mungu ili kweli aweze kuwa ni chombo cha haki, amani, upatanisho na upendo wa kweli!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.