2017-02-17 07:19:00

Parokia ya Mt. Maria Josefa inamsubiri Papa Francisko kwa shauku!


Baba Mtakatifu Francisko baada ya Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu uliokazia kwa namna ya pekee, tafakari kuhusu huruma ya Mungu inayomwilishwa katika maisha na utume wa Kanisa, anaendelea kutembelea Parokia mbali mbali za Jimbo kuu la Roma, ili kukutana na familia ya Mungu, kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa pamoja na kuwaimarisha waamini katika imani, matumaini na mapendo, ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa watu wa nyakati hizi.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili ijayo tarehe 19 Februari 2017, Majira ya saa 10: 00 Jioni kwa saa za Ulaya atakutana na kuzungumza na Jumuiya ya Parokia ya Mtakatifu Josefa wa Moyo Mtakatifu wa Yesu, huko eneo la “Ponte Nona” nje kidogo ya mji wa Roma. Hii ni safari ya kumi na tatu kwa Baba Mtakatifu kutembelea Parokia za Jimbo kuu la Roma, ambako atapata nafasi kuadhimisha Sakramenti ya Upatanisho kwa waamini watakaokuwa wamejiandaa kupokea na kuambata huruma ya Mungu katika maisha yao, ataadhimisha Fumbo la Ekaristi takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Itakumbukwa kwamba, Parokia hii kunako tarehe 16 Desemba 2001 ilibahatika kutembelewa na Mtakatifu Yohane Paulo II ambaye pia aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu.

Padre Francesco Rondinelli, Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Josefa wa Moyo Mtakatifu wa Yesu ambaye amateuliwa hivi karibuni anasema kwamba, wamepokea taarifa ya kutembelewa na Baba Mtakatifu Francisko kutoka kwa Kardinali Agostino Vallini, Makamu Askofu Jimbo kuu la Roma. Bila shaka kila Paroko anatamani kwamba, siku moja, Khalifa wa Mtakatifu Petro aweze kutembelea Parokia yake, kumbe, hii ni furaha ya familia ya Mungu katika eneo hili.

Parokia hii imezinduliwa hivi karibuni na kuwekwa chini ya ulinzi na tunza ya Mtakatifu Maria Josefa Sancho de Guerra, Mwanzilishi wa Shirika Watawa Watumishi wa Upendo, aliyetangazwa kuwa Mtakatifu kunako tarehe 1 Oktoba 2000 na Ibada ya kutabaruku Kanisa hili ikaadhimishwa na Kardinali Camillo Ruini, tarehe 27 Januari 2001. Padre Francesco Rondinelli kwa sasa anaendelea kujifunza mazingira pamoja na kufahamiana na wanaparokia wake ili kutambua changamoto, matatizo na fursa zilizopo, ili hatimaye, aweze kuibua mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji na kitume Parokiani hapo.

Shirika ya Misaada la Kanisa Katoliki Parokiani hapo, Caritas ni mfano bora wa kuigwa kwa ajili ya huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hii inatokana na ukweli kwamba, kiwango cha umaskini wa hali na kipato ni cha hali ya juu kabisa katika eneo hili pengine hii ndiyo sababu ambayo imemsukuma Baba Mtakatifu Francisko kuwatembelea ili kuwatia shime katika maisha na ushuhuda wao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Hili ni eneo ambalo lina idadi kubwa ya watu wasiokuwa na fursa za ajira na matokeo yake ni baadhi yao kutafuta njia za mkato kwa kujihusisha na biashara pamoja na matumizi haramu ya dawa za kulevya. Kuna watu waaminifu wanaotekeleza dhamana na wajibu wao kwa kuzingatia kanuni maadili na utu wema, hawa wamekuwa ni chachu ya kuyatakatifuza maeneo haya kwa njia ya mfano wao bora wa maisha ya Kikristo na kiutu.

Paroko anasema yuko karibu sana na wanaparokia yake, ili kuwasaidia kiroho na kimwili, tayari kuwa ni mashuhuda wa huruma ya Mungu inayoganga na kuponya magonjwa na udhaifu wa mwanadamu. Parokia inaendeleza katekesi makini inayogusa hali halisi ya maisha ya wanaparokia, ili kuweza kukabiliana na changamoto zote hizi kwa mwanga wa Injili ya Kristo! Ni muda wa kufahamiana ili hatimaye kujenga madaraka ya kuwakutanisha watu, ili kusaidiana kwa hali na mali kukabiliana na changamoto za maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.