2017-02-17 09:03:00

Iweni watakatifu kama Baba yenu wa mbinguni!


Wapendwa Taifa la Mungu, tuanze tafakari yetu ya leo tukiongozwa na maisha ya kiroho ya Mtakatifu Maria Goretti. Huyu aliuawa akiwa na miaka 11. Alimkatalia hitaji lake mdhalimu aliyetaka kumbaka.  Huyo alimchoma kisu na kumuua. Akiwa anakata roho Maria Goretti alisali hivi: Ee Mungu msamehe kosa lake. Namtaka mbinguni. Hapa tunaona jinsi nguvu ya msamaha inavyoshinda ubaya wa dhambi. Huu ndio utakatifu wa kimungu.   Katika Neno la Mungu dominika hii ya leo tunaona sheria mbili kinzani. Moja ni katika kitabu cha Wal. 24:19-20 – na mtu akimwumiza mwenziwe, atatendewa kama alivyotenda. Jeraha kwa jeraha, jicho kwa jicho, jino kwa jino. Hasara aliyomtia mwenziwe ndiyo atakayotiwa yeye na nyingine kutoka injili ya Mt. 5:38-39 – mmesikia ya kuwa imenenwa, jicho kwa jicho, jino kwa jino. Mimi lakini nawaambieni, msibishane na mtu mbaya, bali mtu akikupiga shavu la kulia, umwelekezee pia jingine. Utakatifu kama tuonavyo katika somo la kwanza ni kuwa na upendo kwa Mungu kupitia watu wake. Masharti ya upendo anayosema Yesu katika Injili yaweza kuonekana kuwa ni upuuzi. Mtume Paulo katika somo la pili anasema wazi kuwa kwa mwanadamu yaweza kuonekana kuwa ni ujinga.

Ndugu wapendwa, dhana ya dhambi na utakatifu inagusa sana maisha yetu. Sote au wengi wetu tunatambua wazi jinsi ilivyo vigumu kwanza kutambua na pili  kukiri kosa/dhambi na/au kuwajibika kwa makosa/dhambi mbalimbali anazotenda mtu. Mojawapo ya mifano iliyo wazi katika Biblia ni ile dhambi ya mfalme Daudi. Hata wakati nabii Nathan anamsimulia ule mfano, yeye hakung’amua kuwa ullimlenga yeye. Na jibu lake Daudi ni kuwa mtu huyo anastahili kufa. Ni baada tu ya nabii kumwambia kuwa mtu huyo ni wewe, basi anarudi katika fahamu zake. Bahati yake Daudi alikiri kosa lake na kuomba msamaha. Anarudia tena sote tunatambua jinsi ilivyo vigumu kukiri, kukubali au kukiri kosa/dhambi.

Pia sote au wengi wetu tunaona jinsi ilivyo vigumu kupatana na adui zetu. Pengine tuunaona jinsi watu wanavyohangaika au kutumia muda mwingi kulipa kisasi kwa waliowakosea. Au jinsi mtu anavyohangaika kutafuta haki ikiwa amekosewa. Sote pia tunatambua jinsi ilivyo hatari ambapo katika kutafuta haki huko kunavyoweza kupelekea hata kumdhuru mwingine. Hutokea pia hata hilo hitaji la kutafuta haki likaongeza uadui zaidi. Pengine hapa ndipo sheria ya Kristo ya kupendana inapata maana kubwa. Anayependa anatoa upendo. Asiyependa hawezi kutoa kwa vile hana. Tunaambiwa kuwa huwezi kupenda bila kutoa ingawa unaweza kutoa bila kupenda.

Wengi wetu hujiuliza hivi kweli inawezekana kumsamehe adui? Kwenye filamu – “Mission” – tunaona habari juu ya wale watu waliofundishwa dini vizuri na wamisionari Wajesuiti. Baada ya kuhakikisha kuwa wamekomaa katika imani msingi, waliondoka kwenda kufundisha wengine. Baada ya miaka kadhaa wakarudi kuwatembelea wale watu na wakakuta vita vikali vinapiganwa dhidi ya maadui zao huku kukiwa na mauaji mengi kati yao. Yule mmisionari akawakumbusha wale watu – mbona tuliwafundisha msiue? Jibu lao kwa padre likawa sasa mbona wao wanatuua? Hata sisi hapa tunaweza kusema sasa mbona huyu amenikosea au ananikosea daima? Nifanyeje?

Abraham Lincoln, Rais wa 16 wa Marekani anatupata uwezekano wa kuishi msamaha na upatanisho. Wakati akifanya kampeni alitokea mpinzani aliyefanya kila aina ya mbinu ili kuharibu jina na sifa yake. Huyu aliitwa Edwin McMasters Stanton. Alikuwa tayari kufanya lo lote ili Lincoln asipate nafasi ya kushinda uchaguzi wa urais. Hata hivyo Lincoln alishinda na alipokuwa anaandaa Baraza la mawaziri, jina la Stanton likawepo. Wasaidizi wa Rais walifanya juhudi kubwa ila bila mafanikio kumweleza Rais chuki aliyokuwa nayo Stanton dhidi yake. Hata hivyo, Rais alionekana kuzijua wazi mbinu mbaya za Stanton dhidi yake wakati wa kampeni. Rais akasema huyu ananichukia mimi ila siyo Marekani. Huyu ana sifa za kuongoza Marekani na  watu wake. Akamfanya waziri wa ulinzi. Stanton aliposikia uteuzi wake alishangaa mshangao mkubwa. Akakubali ule wadhifa na akaifanya hiyo kazi kwa weledi mkubwa. Lincoln aliuawa. Wakati wa maziko yake Stanton alisema hakika huyu asingeondoa chuki yake dhidi yangu, leo hii angezikwa huku akiacha adui duniani. Lakini kwa vile roho yake ilikuwa tofauti na yangu ameacha rafiki duniani.

Sisi tunaomwamini Mungu hatuna budi kuwa macho katika kutoa majibu ya shida zetu dhidi ya adui zetu. Ndipo hapa Mt. Augustino anatufundisha kuepuka mazingira yanayotupelekea kutenda dhambi, yanayotutia vishawishini au majaribuni. Pia tunakumbushwa kuwa hatuwezi kutenda dhambi kwa vile fulani katenda au anatenda dhambi. Yesu atuambia daima – muwe watakatifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyo Mtakatifu.

Naye mhubiri maarufu Padre Munachi anatutafakarisha kuangalia mitindo yetu ya maisha. Kuishi kwa mazoea au kutokujali.  Anatumia sehemu ya Injili ya Lk. 7:11-17, ambapo tunasikia habari ya binti wa Naim aliyefariki na watu wanapita kwenda kuzika. Amefariki, kwa hiyo kinachofuata ni maziko. Yesu anafanya kinyume. Alikuwa na msafara wake na wao walikuwa na msafara wao. Anatambua hali ya yule mama. Yesu anaweka mkono wake juu ya lile jeneza. Yule mama anatambua nguvu ya Yesu na anasimama. Anatambua katika Kristo uwepo wa uzima dhidi ya kifo. Yesu anasema acha kulia – Lk. 7:11. Kama yule mama asingeshiriki tendo hili, hakika mwanae asingepata uzima. Aliamini na kutambua uzima uliokuwepo na akampatia Mungu nafasi ya kugusa maisha yake. Ndugu zangu, Mwenyezi Mungu ametupatia nafasi ya kushiriki utakatifu wake. Tuna uwezo wa kufanya miujiza tukiwa upande wake Mungu.

Ndugu zangu, tulipoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu tulitafakarishwa na Neno la Mungu na kualikwa kuwa watu wa matendo na tukawajibishwa kuishi Neno la Mungu kwa matendo. Ilit tuweze kuenzi Neno la Mungu dominika hii, hatuna budi kuutafakari ule wajibu wetu wa Kikristo.  Yako matendo ya nje ya kimwili ya huruma – kuwalisha wenye njaa, kuwanywesha wenye kiu, kuwavika walio uchi, kuwakaribisha wageni, kuwaponya wagonjwa, kuwatembelea wafungwa na kuwazika wafu na matendo ya huruma ya kiroho ambayo ni kuwashauri wenye mashaka, kuwaelekeza wasiojua (wajinga), kuwaonya wadhambi, kuwafariji walioonewa, kuwasamehe wakosefu  (waliotukosea), kuwavumilia wakorofi na wasumbufu na kuwaombea wazima na wafu. Tukifanya hivi tutavuka ile hali ya kifarisayo na kutenda tendo la huruma kama anavyotutaka Bwana katika Injili ya leo.

Katika Mt. 18:21 – kuhusu kusameheana tunasoma hivi, kisha Petro akamwendea, akasema, Bwana, ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? Mtume Petro hakusema aliyenikosea aniombe msamaha mara ngapi. Tunakumbuswa kuwa tendo halisi la upatanisho hutoka kwa Mungu, kwa njia ya mwanawe na mtume Paulo anasema kuwa naye Mungu anatupa sisi huduma ya upatanisho – 2Kor. 5:18. Nasi tunaalikwa tukasemeheane makosa yetu.  

Tumsifu Yesu Kristo.

Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.