2017-02-16 09:20:00

Washindi wa tuzo ya kimataifa: uchumi na jamii!


Kardinali Reinhard Marx, Rais wa Jopo la Tuzo la Kimataifa la “Jamii na Uchumi” linalotolewa na “Mfuko wa Centesimus annus - Pro Pontefice” kwa ajili ya kuhamasisha uelewa wa Mafundisho Jamii ya Kanisa, amewatambulisha washindi wa Tuzo hii kwa Mwaka 2017, Jumatano tarehe 15 Februari 2017 wakati alipokuwa anazungumza na waandishi ya habari mjini Vatican. Tuzo ya Kimataifa imetolewa kwa Markus Vogt kutoka Ujerumani ambaye amejipambanua kwa namna ya pekee katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Katika kitabu chake Markus Vogt anakazia kwa namna ya pekee mambo makuu matatu yaani: uchumi, ekolojia na masuala jamii; kama mambo msingi yanayokamilishana katika mchakato wa kupambana na umaskini duniani, binadamu na mahitaji yake msingi akipewa kipaumbele cha kwanza. Anakazia umuhimu wa umoja na mshikamano katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu, ili kuweza kumletea mwanadamu maendeleo endelevu yanayofumbatwa katika kanuni auni!

Kardinali Reinhard Marx anaendelea kusema kwamba, tuzo kwa waandishi wa habari waliojipambanua katika kazi yao mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa inakwenda kwa Padre Dominique Greiner, Jaalim na Mhariri mkuu wa Jarida la “La Croix” linalochapishwa kwa lugha ya Kifaransa. Katika wavuti yake iliyogawanyika katika sehemu kuu sita, anapembua kwa kina na mapana Mafundisho Jamii ya Kanisa kuhusu: Ekolojia na maisha; Umaskini na uhamiaji; Uchumi, soko, biashara na kazi; Siasa na mafao ya wengi”, Vita, amani, ugaidi na sehemu ya mwisho inajikita katika masuala mchanganyiko! Wavuti hii inajipambanua kwa kuwa na mvuto kwa watu wanaotaka kujitajirisha kwa namna ya pekee na Mafundisho Jamii ya Kanisa, ili kuweza kujenga na kudumisha Jamii inayojikita katika haki, udugu na mshikamano!

Kardinali Reinhard Marx anasema, mwandishi habari wa tatu aliyetunukiwa tuzo hii ni Oswald Schafers, mtangazaji mahiri ambaye amefanikiwa katika kazi yake kumtambulishwa Oswald von Nell-Breuning aliyeishi kati ya Mwaka 1890 – 1991. Hawa ni kati ya Magwiji wa Mafundisho Jamii ya Kanisa kwenye karne yak umi na tisa. Ni mtunzi wa kazi inayojulikana kama “Quadragesimo anno di Pio XI, mwaka 1931”. Mtangazaji huyu pamoja na mambo mengine anakazia umuhimu wa kanuni msingi za Mafundisho Jamii ya Kanisa yaani: Kanuni auni, utu na heshima ya binadamu na mshikamano, kwa kuonesha umuhimu wa Mafundisho Jamii ya Kanisa ndani na nje ya Ujerumani.

Kwa upande wake Dr. Domingo Sugranyes Bickel, Rais wa “Mfuko wa Centesimus annus - Pro Pontefice”, amefafanua kuhusu Kongamano la Kimataifa la“Mfuko wa Centesimus annus - Pro Pontefice” litakalofanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 18 – 20 Mei 2017. Ni Kongamano linalotarajiwa kuhudhuriwa na wajumbe 250 kutoka katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu pamoja na wataalam wa Mafundisho Jamii ya Kanisa. Kongamano hili litaongozwa na kauli mbiu “Utengenezaji wa fursa za ajira, ukamilifu wa binadamu katika kipindi cha digitali; motisha kwa mshikamano na tunu msingi za kijamii. Hawa ni wajumbe watakaotoka katika nchi 19 duniani, kama sehemu ya mchakato wa mapambano dhidi ya baa la umaskini. Katika kipindi cha mwaka mzima, Mfuko huu umejitahidi kuhamasisha mapambano dhidi ya umaskini duniani; umuhimu wa uchumi wa kidigitali kujielekeza zaidi katika huduma kwa mafao ya wengi.

Itakumbukwa kwamba, Mfuko huu ulianzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II aliyetaka usaidie kuragibisha ufahamu ya Mafundisho Jamii ya Kanisa, shughuli mbali mbali zinazofanywa na Vatican katika medani mbali mbali za maisha ya binadamu kwa ajili ya: mafao ya wengi, mafungamano na maendeleo endelevu ya binadamu; utengenezaji wa fursa za ajira pamoja na kuendeleza mchakato wa uwekezaji katika rasilimali watu! Tuzo la Kimataifa la “Jamii na Uchumi” hutolewa na “Mfuko wa Centesimus annus - Pro Pontefice” kila baada ya miaka miwili. Mfuko huu tangu mwaka 2010 umechangia kiasi cha millioni mbili kwa ajili ya huduma ya upendo inayotolewa na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Hii ni ada na mchango mbali mbali unaotolewa na wajumbe pamoja na wasamaria wema, ili kuliwezesha Kanisa kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo na mshikamano na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.