2017-02-15 16:54:00

Yaliyojiri kwenye ziara ya Askofu mkuu Gallagher nchini Czech!


Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican, kuanzia tarehe 9 - 11 Februari 2017 amefanya ziara ya kikazi huko Prague, Jamhuri ya Watu wa Czech kwa mwaliko wa Bwana Lubomir Zaoràlek, Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Jamhuri ya Watu wa Czech. Askofu mkuu Gallagher pamoja na ujumbe wake, alipata nafasi ya kukutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki Jamhuri ya Watu wa Czech.

Mazungumzo kati ya Askofu Mkuu Gallagher na Bwana Lubomir Zaoràlek yamegusia uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Jamhuri ya Watu wa Czech na kuridhishwa na hatua ambayo imefikiwa hadi wakati huu, mintarafu mahusiano kati ya Serikali na Kanisa Katoliki ambalo kimsingi limekuwa mstari wa mbele katika utoaji wa huduma za kijamii hususan katika sekta ya elimu, afya, ustawi na maendeleo endelevu ya jamii. Ni matumaini ya viongozi hawa wawili kwamba, sasa kuna haja ya kupiga hatua nyingine zaidi kwa kutiliana sahihi itifaki ya makubaliano kati ya nchi hizi mbili.

Imekuwa ni fursa kwa viongozi hawa kujadiliana kuhusu wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi Barani Ulaya; Vitendo vya kigaidi na madhara yake; hatima ya Umoja wa Ulaya kwa siku za usoni; vita, kinzani na mipasuko huko Mashariki ya Kati; mchakato wa maendeleo endelevu Barani Afrika na mwishoni, Serikali ya Jamhuri ya Watu wa Czech imerudia tena kutoa mwaliko kwa Baba Mtakatifu Francisko ili aweze kuitembelea na kuwaimarisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo.

Askofu mkuu Gallagher alipata nafasi pia ya kuzungumza na Bwana Daniel Herman, Waziri wa utamaduni na ushirikiano kati ya Serikali na Viongozi wa kidini, ambaye ameridhishwa na uhusiano na ushirikiano wa karibu uliopo kati ya Serikali na Kanisa, kwa kueleza kwamba, Kanisa linamiliki asilimia 44 ya vivutio vyote vya kitalii nchini humo vyenye asili ya mambo matakatifu. Viongozi hawa wameridhishwa na hatua ya Serikali kurejesha tena kwa Kanisa mali iliyokuwa imetaifishwa na Serikali wakati wa utawala wa Kikomunisti na kwamba, kwa sasa Kanisa linaendeleza mchakato wa Uinjilishaji mpya kwa kasi na mwamko mkubwa zaidi. Wamridhishwa pia na ushirikiano wa kiekumene kati ya Makanisa ya Kikristo nchini Czech.

Askofu mkuu Gallagher alikutana na kuzungumza na viongozi wa Kanisa Katoliki waliokuwa chini ya uongozi wa Kardinali Dominic Duka, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Jamhuri ya Watu wa Czech. Katika mazungumzo yao, wamegusia tema mbali mbali katika maisha na utume wa Kanisa; uhusiano kati ya Kanisa na Serikali; dhamana, wajibu na utume wa Kanisa mahalia; matatizo, changamoto na fursa zilizopo katika mchakato wa Uinjilishaji mpya; changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji nchini humo; upendo na mshikamano na Wakristo huko Mashariki ya Kati. Ziara hii ya kikazi iliyofanywa na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher ilipania pamoja na mambo mengine kuimarisha uhusiano kati ya Vatican na Jamhuri ya Watu wa Czech, kwa matarajio ya kuboresha zaidi uhusiano baina ya pande hizi mbili!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.