2017-02-15 16:36:00

Mafungo ya Kwaresima 2017: Fumbo la Pasaka!


Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kadiri ya Injili ilivyoandikwa na Mtakatifu Mathayo, ndiyo tema iliyochaguliwa na Padre Giulio Michellin kwa ajili ya Mafungo ya kiroho kwa Baba Mtakatifu Francisko pamoja na viongozi wake waandamizi kutoka Sekretarieti kuu ya Vatican, maarufu kama “Curia Romana”. Mafungo haya yataanza tarehe 5 hadi 10 Machi 2017 huko Ariccia, nje kidogo ya mjini wa Roma. Hii ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu, Siku kuu inayotanguliwa na Siku 40 za Mfungo wa Kipindi cha Kwaresima: muda wa kusali, kutafakari, kufunga na kutenda matendo ya huruma.

Itakumbukwa kwamba, kauli mbiu inayoongoza ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2017 ni “Neno ni zawadi; jirani yako ni zawadi pia”. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujitahidi kumwilisha ile sehemu ya Injili ya Lazaro Maskini na tajiri asiyejali!

Padre Giulio Michellini, mwenye umri wa miaka 53 ni Mkapuchini aliyeweka nadhiri zake za daima 1992 na kupewa Daraja Takatifu ya Upadre mwaka 1994. Ni mtaalam wa lugha kutoka Chuo kikuu cha Perugia, Italia, lakini zaidi ni bingwa wa Taalimungu ya Biblia, ujuzi aliojipatia kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian na Yerusalemu ambako alijipatia Shahada ya Uzamivu. Ni mkurugenzi wa Jarida la la “Convivium Assisiense” na mwandishi maarufu wa makala mbali mbali za kitaifa na kimataifa.

Ratiba elekezi inaonesha kwamba, mafungo haya yatafunguliwa rasmi Jumapili jioni tarehe 5 Machi 2017 majira ya saa 12: 00 jioni kwa saa za Ulaya kwa Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu pamoja na Masifu ya Jioni. Kwa siku nyingine zinazofuatia, Baba Mtakatifu na jirani zake katika mafungo watakuwa wanaianza siku kwa Ibada ya Misa Misa Takatifu saa 1: 30. Tafakari ya kwanza itakuwa inatolewa saa 3: 30, Tafakari ya Pili ni saa 10: 00 za Jioni na baadaye itafuatia Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu pamoja na Masifu ya Jioni. Ijumaa, tarehe 10 Machi 2017, kutakuwepo na mabadiliko ya ratiba, kwani kutakuwa na tafakari moja tu kwa siku.

Padre Giulio Michellini anasema, mafungo haya yataanza kwa tafakari juu ya ushuhuda wa Mtakatifu Petro kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu aliye hai. Baadaye wataendelea kutafakari kuhusu maneno ya mwisho yaliyotolewa na Kristo Yesu mwanzoni kabisa wa mateso yake. Mkate na Mwili wa Kristo; Divai na Damu Azizi ya Yesu; Sala ya Yesu bustanini Gethsemane pamoja na kukamatwa kwa Yesu. Yuda Iskarioti na vile vipande thelathini vye fedha vilivyotumika kununulia konde la mfinyanzi liwe mahali pa kuzikia wageni.

Mchakato wa kesi ya Yesu mbele ya Mahakama ya Kirumi, ushauri wa mke wa Pilato na ndoto ya Mungu. Kiini cha tafakari hii ni kifo cha Masiha, kuzikwa kwake na maana ya Jumamosi ya Masiha, hatimaye, Kaburi tupu, ufufuko wa Kristo Yesu na hatimaye, Padre Giulio Michellini atatoa hitimisho kama muhtasari wa mambo makuu aliyotaka kukazia katika mafungo haya ambamo Baba Mtakatifu Francisko pamoja na waandamizi wake wa karibu watashiriki kikamilifu, ili kujichotea nguvu na ari ya kusonga mbele katika maisha na utume wao. Itakumbukwa kwamba, wakati wote wa Mafungo, mikutano yote ya faragha na katekesi zitasitishwa kwa muda. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican itaendelea kukushirikisha yale yatakayokuwa yanajiri kwenye mafungo hayo ya Baba Mtakatifu Francisko na waandamizi wake wa karibu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.