2017-02-14 11:20:00

Papa Francisko kwa Maaskofu wa Costa Rica: Waonjesheni watu upendo!


Costa Rica ni kati ya nchi za Amerika ya Kusini zinazokabiliwa kwa kiasi kikubwa la janga la kuwafanyisha watoto kazi za suluba na hivyo kuwakuta watoto wakiishi katika mazingira magumu na hatarishi kwa afya, usalama na makuzi yao. Umaskini wa hali na kipato ni chanzo kikuu kinachopelekea wanafunzi wengi kushindwa kuhitimu masomo yao kuanzia hata katika shule za msingi, hali inayoendelea kuwatumbukiza watu wengi katika baa la umaskini, ujinga na maradhi. Costa Rica inakabiliwa na changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kutoka: Colombia, Venezuela, Guatemala, Honduras, El Salvador na Cuba. Biashara haramu ya dawa za kulevya ni changamoto kubwa na endelevu huko Costa Rica.

Hizi ni changamoto kubwa katika maisha na utume wa Kanisa ambazo zimebainishwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Costa Rica ambalo limeanza hija ya kitume inayofanywa na Maaskofu Katoliki walau kila baada ya miaka mitano mjini Vatican. Maaskofu wa Costa Rica, Jumatatu, tarehe 13 Februari wamepata fursa ya kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko na kwamba, hija hii ya kitume itahitimishwa hapo tarehe 17 Februari 2017. Hii pia ni nafasi ya kufanya hija kwenye kaburi la Mtakatifu Petro na kukutana na viongozi waandamizi wa Sekretarieti kuu ya Vatican.

Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Askofu Oscar Fernandez Guillèn, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Costa Rica anasema, matatizo na changamoto ni sehemu ya maisha na utume wa Kanisa, lakini wanamshukuru Mungu kwani kuna idadi kubwa ya miito mitakatifu inayosaidia kutoa huduma makini kwa familia ya Mungu Amerika ya Kusini. Mapadre na watawa wameendelea kuwa mstari wa mbele kupeleka Furaha ya Injili kwa watu walioko pembezoni mwa jamii, kwa kukazia zaidi: katekesi, majiundo awali na endelevu kwa waamini walei pamoja na kuwahamasisha waamini kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya utakatifu wa maisha, kielelezo cha imani tendaji! Waamini wanahamasishwa kuwa ni mashuhuda wa Injili ya familia inayofumbatwa katika Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Baraza la Maaskofu Katoliki Costa Rica limejiwekea mbinu mkakati wa malezi awali na endelevu kwa wanandoa watarajiwa ili kuhakikisha kwamba, wanatambua: ukuu, uzuri na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia, tayari kuutolea ushuhuda katika maisha yao kama kielelezo cha imani tendaji. Familia zinatakiwa kusimama kidete dhidi ya utamaduni wa kifo kwa kukumbatia Injili ya uhai, tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Katekesi makini na endelevu ni dawa mchunguti dhidi ya ukanimungu, mawazo mepesi mepesi na utepetevu wa kiimani. Kumbe, waamini walei wanawajibika kuwa ni watetezi wa tunu msingi za maisha ya kikristo, kiutu na kijamii.

Kanisa Katoliki nchini Costa Rica linakabiliana na changamoto, matatizo na fursa mbali mbali zinazoendelea kujitokeza kwa kujikita katika: Mafundisho Jamii ya Kanisa, msisitizo ukiwa ni utu, heshima, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Sera na mikakati ya kiuchumi haina budi kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mahitaji msingi ya binadamu, chachu na kikolezo cha maendeleo endelevu. Elimu makini ni tema inayoendelea kuvaliwa njuga na Maaskofu wa Costa Rica ili kuwapatia watoto na vijana; elimu, ujuzi, maarifa na stadi za maisha ili kupambana na mazingira, tayari kuwa na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Sera na mikakati ya shughuli za kichungaji inazingatia pia umuhimu wa Katekesi na elimu ya dini shuleni kama sehemu ya mchakato wa makuzi na malezi kwa watoto na vijana wa kizazi kipya!

Familia ya Mungu nchini Costa Rica inaendelea kuonesha moyo wa upendo, ukarimu na kuwajali wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta. Usalama, hifadhi na maisha bora zaidi nchini humo. Lakini, wakimbizi na wahamiaji hawa kwa sasa wanakabiliana na changamoto kubwa kwani Marekani na Nicaragua zimefunga malango yake kwa kujenga ukuta. Hata hivyo, Costa Rica inaendelea kutoa hifadhi ya kisiasa kwa wakimbizi na wahamiaji kutoka Cuba, Haiti na baadhi ya nchi za Kiafrika. Serikali inaonesha mshikamano kwa kujali na kuguswa na mahangaiko ya watu hawa. Baraza la Maaskofu Katoliki Costa Rica linampongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro; kwa kuonesha huruma kama Baba wa mbinguni; imani na upendo katika maisha na utume wake. Papa Francisko ni kiongozi ambaye yuko karibu pamoja na watu, mfano bora wa kuigwa katika utekelezaji wa sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa familia ya Mungu nchini Costa Rica!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.