2017-02-13 10:00:00

Pd. Trille Kuku Andali ateuliwa kuwa Askofu wa Jimbo la El Obeid


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Mheshimiwa Sana Padre Yunan Tombe Trille Kuku Andali kuwa ni Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la El Obeid nchini Sudan Kongwe. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mteule ambaye ni mzaliwa wa Jimbo Katoliki la El Obeid alikuwa ni Gombera wa Seminari kuu ya Mtakatifu Paulo, Juba, Sudan ya Kusini. Itakumbukwa kwamba, Askofu mteule alizaliwa tarehe Mosi Januari 1964 Jimboni El Obeid. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, kunako tarehe 7 Aprili 1991 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre.

Mara baada ya Upadrisho, Askofu mteule Yunan Tombe Trille Kuku Andali kati ya mwaka 1991 hadi mwaka 1995 alibahatika kufanya kazi katika Parokia za El Nahud, Nayala El Fasher na Kadaguli. Kuanzia mwaka 1995 hadi mwaka 2002 aliteuliwa kuwa Gombera wa Seminari Ndogo ya El Obeid, wakati huo akiwa pia Makamu Askofu Jimbo Katoliki El Obeid. Kati ya Mwaka 2002 hadi mwaka 2009 alitumwa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Afrika Mashariki, CUEA kwa ajili ya masomo ya juu ya Sheria za Kanisa na hatimaye, kujipatia Shahada ya uzamivu.

Baada ya kurejea nchini Sudan Kongwe, kuanzia mwaka 2009 hadi mwaka 2012 aliteuliwa kuwa Paroko wa Parokia ya Watakatifu Wote huko Saraf Jamus. Na kunako mwaka 2012 hadi kuteuliwa kwake kuwa Askofu Mpya wa Jimbo la El Obeid amekuwa ni Gombera wa Seminari kuu Mtakatifu Paulo, Juba, Sudan ya Kusini. Itakumbukwa kwamba, Jimbo Katoliki la El Obeid ni sehemu ya Jimbo kuu la Khartoum, Sudan Kongwe, lililoanzishwa kunako mwaka 1974. Hadi sasa kuna Parokia 14 zinazohudumiwa na Mapadre 30 kati yao kuna Mapadre 24 wa Jimbo na Mapadre 6 ni watawa. Kuna watawa 19 na Majandokasisi 15 wanaoendelea kupata majiundo kwenye Seminari kuu. Jimbo Katoliki la El Obeid limekuwa wazi tangu mwezi Agosti 2015, baada ya Baba Mtakatifu Francisko kumteuwa Askofu Michael Didi Adgum Mangoria kuwa Askofu mwandamizi wa Jimbo kuu la Khartoum, Sudan Kongwe.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.