2017-02-13 14:34:00

Ghadhabu, wivu na visasi vinabomoa udugu na mshikamano!


Wivu usiokuwa na mvuto wala mashiko, chuki na uhasama ni kati ya mambo madogo madogo yanayobomoa mafungamano ya kifamilia, changamoto kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kudhibiti mambo haya mapema iwezekanvyo, kwani yanavuruga udugu na mshikamano kama ilivyotokea kwa Kaini aliyeghadhabika sana na uso wake kukunjamana kama kigae baada ya Mungu kutoridhishwa na sadaka iliyotolewa na Kaini. Na kwa mara ya kwanza neno “ndugu yako” linatumika katika Maandiko Matakatifu. Huu ni udugu uliopaswa kukuzwa na kudumishwa, lakini ukasitishwa kutokana na wivu usiokuwa na mashiko, kiasi cha kushindwa kabisa kudhibiti na kuizuia dhambi hii!

Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Jumatatu, tarehe 13 Februari 2017. Ibada hii imehudhuriwa pia na Makardinali Washauri wakuu walioanza kikao chao cha kumi na nane mjini Vatican. Baba Mtakatifu ametolea Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumsindikiza Padre Adolfo Nicolàs aliyekuwa Mkuu wa Shirika la Wayesuit kuanzia mwaka 2008 hadi mwaka 2016. Baba Mtakatifu amemshukuru na kumpongeza kwa utume wake wakati akiwa Mkuu wa Shirika na sasa anamtakia heri na baraka katika maisha na utume mpya huko Mashariki ya Kati.

Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kaini badala ya kudhibiti ghababu aliyokuwa nayo dhidi ya ndugu yake Abel, akaimeza na kuendelea kuipika moyoni mwake kiasi hata cha kusababisha mauaji ya ndugu yake. Hivi ndivyo inavyotokea hata katika maisha ya kawaida, watu wanaanza kidogo kidogo kuwekeana kisasi na uadui; chuki na uhasama kiasi hata cha kugeuka kuwa ni banzi lilovunjilia mbali mafungamano ya kidugu na udugu.

Baba Mtakatifu anawakumbusha waamini kwamba, ghabahu ni dhambi inayoweza kumwambata mwamini, ikamtesa na kukua kiasi cha kusababisha maafa makubwa. Ghaghabu inasababisha mpasuko na kujenga uhasama kati ya ndugu na matokeo yake kusambaratisha familia na jamii katika ujumla wake. Baada ya kutenda yote haya, mtu anagundua kwamba, hana tena ndugu, amejitenga na kubaki mpweke kama mti wa Mchongoma. Kumbe, kuna haja ya kudhibiti ghadhabu kwani ni kinyume kabisa cha Ukristo kwani madhara yake ni makubwa. Ni kweli kuna mateso na mahangaiko ya ndani, haya ni sawa anasema Baba Mtakatifu lakini ghadhabu ni kinyume cha Ukristo!

Hata katika maisha ya kawaida ndani ya Kanisa kuna wakati wivu na ghadhabu vinajitokeza kiasi cha kuanza kuhatarisha maisha na utume wa Kanisa; umoja na mshikamano wa kidugu. Mwenyezi Mungu akamuuliza Kani “Yuko wapi ndugu yako?” naye akamjibu Mwenyezi Mungu “Sijui, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?” Mwenyezi Mungu akamwambia kwamba, sauti ya damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi. Baba Mtakatifu anasema, ni kweli kabisa watu wanaweza kujigamba kwamba, hawajahi kufanya mauaji, lakini ukiwa na mawazo mabaya juu ya ndugu na jirani yako, tayari umekwisha kutenda dhambi hii kwa njia ya mawazo, kwa kumtenga na kumbagua na matokeo yake ni vita na mauaji ambayo yanaanza kama kitu kidogo tu.

Kuna watu ambao hawaguswi na maafa yanayosababishwa na mabomu, lakini ikumbukwe kwamba, hata leo hii kuna damu ya watu wasiokuwa na hatia inayoendelea kumlilia Mungu kutoka ardhini. Hii ni damu ambayo ina uhusiano wa karibu na wivu, ghadhabu na kijicho kisichokuwa na mvuto wala mashiko, kiasi hata cha kuvuruga na kubomoa udugu. Baba Mtakatifu anawataka waamini kusikiliza tena lile swali na Mungu anayewauliza, Je, yuko wapi ndugu yako? Wamwombe neema ya kudhibiti ndimi zao ambazo zina makali kuliko ncha ya upanga, ili kuweza kujenga na kudumisha umoja na udugu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.