2017-02-11 10:46:00

Yaliyojiri kwenye mkutano kati ya Papa Francisko na Watawa!


Kanisa daima linahamasishwa kutoka katika ubinafsi wake, ili kuwaendelea watu huko waliko, tayari kuwatangazia Injili ya matumaini, furaha na upendo. Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo linataka kuwasikiliza vijana na kuwasaidia kupambana na changamoto za maisha, ndiyo maana Baba Mtakatifu Francisko ameitisha Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana itakayoadhimishwa mwaka 2018 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya miito”.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, watawa watashiriki kikamilifu katika mchakato wa maandalizi na hatimaye, maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana. Itakumbukwa kwamba, katika kipindi cha miaka mitatu kama sehemu ya maandalizi ya kilele cha Siku ya Vijana Duniani, itakayoadhimishwa nchini Panama kunako mwaka 2019, vijana watasindikizwa kwa tafakari ya Bikira Maria. Nguvu ya kuweza kukabiliana na changamoto katika maisha na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro inapata chimbuko lake katika imani na matumaini kwa Kristo Yesu, alfa na omega, mwanzo na mwisho wa yote!

Watawa wanapaswa kushuhudia unabii kwa njia ya maisha, wito na utume wao miongoni mwa familia ya Mungu, daima wakiendelea kukuza na kudumisha maisha ya kijumuiya, kifungo cha umoja, upendo na mshikamano wa dhati. Kuna haja ya kuendelea kuboresha mahusiano mema kati ya watawa na Maaskofu mahalia kwa kutegemezana na kukamilishana katika maisha na utume wa Kanisa. Nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ni kashfa kubwa ndani ya Kanisa, changamoto ni kutubu na kumwongokea Mungu.

Haya ni kati ya mambo mazito yaliyozungumzwa na Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 25 Novemba 2016 alipokutana na wakuu wa mashirika ya kitawa na kazi za kitume 140 waliokuwa wamehitimisha mkutano wao mkuu wa themanini na nane. Ni mkutano ambao ulidumu kwa muda wa masaa matatu kamili. Walipata muda wa mapumziko na hatimaye, Baba Mtakatifu akasalimiana na kila mmoja wao. Baba Mtakatifu alitaka mkutano huu uwe huru, wazi na wa kidugu, ili kuliwezesha Kanisa kusonga mbele kwa imani na matumaini, licha ya mapungufu yanayojionesha miongoni mwa watoto wake! Mkutano huu uliongozwa na Padre  Mario Johri, Rais wa Umoja wa Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume pamoja na Padre David Glenday, Katibu mkuu wa umoja huo!

Baba Mtakatifu anasema, baada ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia, Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu ilipendekeza tema za kufanyiwa kazi na Maaskofu kwa Sinodi iliyokuwa inafuata! Kati ya mada zilizopendekezwa ni: vijana majiundo ya kikasisi, majadiliano ya kidini, haki na amani. Wajumbe, wakapembua kwa kina na mapana tema hizi wakati Baba Mtakatifu akiwasikiliza kwa kina, lakini moyoni mwake, akata kukazia umuhimu wa majiundo makini kwa vijana wa kizazi kipya, mang’amuzi ya wito wa Kipadre, ili kuwawezesha Wakleri kupenda na kuthamini maisha na wito wao wa Kipadre, tayari kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa. Mang’amuzi yanawasaidia vijana wa kizazi kipya  kufikiri na kutenda kadiri ya mpango wa Mungu katika maisha yao, huku wakisaidiwa na mwanga wa Injili. Mwishoni, Baba Mtakatifu anasema akaunganisha changamoto hizi na hatimaye, kauli mbiu ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa Mwaka 2018 ikatolewa yaani ”Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito”.

Vijana wanapaswa kusindikizwa katika hija ya maisha ili kutambua mpango wa Mungu na kuutekeleza katika ukomavu wa maisha. Mwongozo wa kutendea kazi wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana umekamilika na tayari kutumwa kwenye Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia, kwa ajili ya utekelezaji wake. Baba Mtakatifu anawaalika viongozi wa Kanisa kuwa karibu sana na vijana katika maisha na utume wao; kwa kuwasikiliza kwa makini na kutenda kwa ajili pamoja na vijana. Uwepo wa watawa katika mchakato wa maadhimisho ya Sinodi ya vijana ni muhimu sana kwani watawa na vijana ni sawa na chanda na pete! Ni watu wanaoshirikiana kwa karibu sana.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, idadi ya watawa katika nchi za Magharibi inaendelea kupungua siku hadi siku na kwamba, hii inatokana pia na idadi ndogo ya watoto wanaozaliwa katika nchi hizi, hali ambayo inatishia maisha na utume wa Kanisa. Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana itajitahidi kutoa majibu kwa changamoto hii. Jambo la msingi ni kujizatiti katika ubora wa maisha na utume wa watawa duniani, wanaosindikizwa na Maaskofu mahalia katika ukuaji wao.

Kwa bahati mbaya, kuna baadhi ya mashirika ambayo yanafumbatwa zaidi katika karama za kibinadamu badala ya karama za Roho Mtakatifu na matokeo yake ni kuporomoka kwa mashirika ya namna hii kutokana na kugubikwa na kashfa na udhaifu wa kibinadamu. Hawa ni watawa ambao kwa macho walionekana kuwa ni mashujaa wa imani, lakini kumbe, ni debe tupu haliachi kutika! Roho Mtakatifu anatenda katika hali ya ukimya na unyenyekevu, ili kuleta mvuto na mashiko kwa waja wake. Watawa waendelee kuwa ni vyombo na mashuhuda amini wa matumaini na Injili ya Kristo kwa familia ya Mungu inayowazunguka. Kanisa kamwe haliwezi kukua na kuongezeka kutokana na wongofu wa shuruti, bali ni kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, ameridhia kwamba, mchakato wa maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 uongozwe na Bikira Maria kwani sehemu kubwa ya familia ya Mungu Amerika ya Kusini ina ibada maalum kwa Bikira Maria. Huyu ni Mama wa Yesu, awasaidie waamini kumkumbatia Yesu nyoyoni mwao; Bikira Maria anayesikiliza kwa makini, kutafakari na kutekeleza mpango wa Mungu katika maisha yake.

Maisha na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro una: furaha, changamoto na kero zake. Baba Mtakatifu anasema, maisha yake si rahisi, lakini jambo la kumshukuru Mungu ni kwamba, tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki, anaishi kwa amani tele, kama maji mtungini! Amejiachilia na kujikabidhi mikononi mwa Kristo Yesu, tangu wakati huo, kamwe hajatindikiwa na amani pamoja na utulivu wa ndani! Wakati wa mikutano elekezi kabla ya uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, Makardinali waligusia kuhusu umuhimu wa kufanya mageuzi ya kina kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican; walikuwa wamenusa harufu ya rushwa na ufisadi ndani ya Vatican.

Pamoja na changamoto zote hizi anasema Baba Mtakatifu Francisko, wakati wa shida na magumu anapenda kujikabidhi kwa Mtakatifu Yosefu; anapenda kuirutubisha siku yake kwa njia ya sala na tafakari ya Neno la Mungu; mambo yanayompatia amani na utulivu wa ndani, lakini kimsingi hii ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Wakuu wa mashirika wajifunze kuteseka kwa ajili ya mafao ya wengi katika hali ya unyenyekevu, tayari kuubeba Msalaba na kumfuasa Kristo Yesu bila kukimbia matatizo kama alivyofanya Ponsio Pilato kwa kunawa mikono wakati wa kumhukumu Kristo Yesu.

Baba Mtakatifu anawataka watawa kuwa mashuhuda wa kinabii kwa njia ya wito, maisha na utume wao unaofumbatwa katika tunu msingi za Kiinjili tayari kuyatakatifuza malimwengu; kama walivyofanya waanzilishi wa mashirika yao. Wawe ni watu wenye kiasi, wanaofunga na kusali; watu huru katika kufikiri na kutenda na kwamba, wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa furaha ya Injili. Watawa watambue kwamba, maisha ya kijumuiya ni toba endelevu inayopaswa kujikita katika huruma, upendo, msamaha na mshikamano. Jumuiya inapaswa kuwa ni mahali pa kusikia na kusikilizana, tayari kusaidia mchakato wa kupyaisha maisha na utume wa Kanisa kwa njia ya ushuhuda wa umoja na mshikamano wa kidugu unaosimikwa katika fadhila ya unyenyekevu!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, kuna haja kwa watawa na Maaskofu mahalia kuboresha mahusiano katika maisha na utume wa Kanisa kadiri ya mwanga wa Waraka wa”Mutuae relationis” uliotolewa kunako mwaka 1978; ukajadiliwa kwenye Sinodi ya Watawa mwaka 1994 na katika mkutano wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume uliofanyika mwaka 2017. Watawa wanapaswa kushirikishwa katika maisha na utume wa Makanisa mahalia, bila kutengwa hata kidogo. Watawa wapewe nafasi ya kumwilisha karama na utume wao kwa Makanisa mahalia, ili pia kuwasaidia Mapadre wa Majimbo kuthamini na kuenzi maisha ya kijumuiya.

Watawa na Mapadre wa Jimbo wajitahidi kufahamiana, ili waweze kuthaminiana na kushirikiana kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo Yesu. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, mgogoro mkubwa kati ya Maaskofu mahalia na watawa ni masuala ya fedha. Sehemu kubwa ya Parokia zinazozimamiwa na kuongozwa na watawa zimekuwa na mafanikio makubwa ikilinganishwa na Parokia zinazosimamiwa na Wakleri wa Majimbo. Kuna tatizo kubwa kwa Maparoko kutoka kwenye Mashirika ya Kitawa kuhamishwa mara kwa mara, hali ambayo inaweza kudhohofisha uhusiano na mafungamano kati ya Askofu mahalia na watawa. Ufukara ni changamoto nyingine inayowatambulisha watawa katika maisha na utume wao. Haya ni mambo ambayo yanapaswa kuangaliwa kwa dhati ili kuendeleza mchakato wa maboresho ya mahusiano kati ya watawa na Maaskofu mahalia.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka watawa kuwa waaminifu, wakweli na watu wazi katika matumizi ya rasilimali fedha, ili kuepukana na kashfa ambazo zimepelekea mashirika mengine ya kitawa kujikuta yanatumbukia katika kashfa za masuala ya fedha. Jambo la msingi kwa watunza fedha wa mashirika wasiwe ni watu wenye uchu wa mali na fedha, kwani ni hatari sana kwa maisha na utume wa Kanisa. Mashirika ya kitawa yawe makini na vitega uchumi vyao na kamwe wasiwekeze kwenye maeneo yanayohatarisha maisha na utume wao. Kashfa za nyanyaso za ngono kwa watoto wadogo anasema Baba Mtakatifu ni vitendo ambavyo vimelichafua sana Kanisa. Huu ni ugonjwa unaopaswa kupewa tiba muafaka, tangu mwanzo kabisa wa kuchagua watakaji kwenye maisha ya kitawa na kipadre; umuhimu wa kujikita katika majiundo makini ya awali na endelevu, lakini zaidi ya yote kuna haja ya kuambata toba na wongofu wa ndani.

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha mkutano wa maswali na majibu pamoja na wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume kwa kuwakumbusha kwamba, Kanisa limeanzishwa ili kutoka kwenda kuwatangazia watu wa Mataifa Injili ya matumaini, upendo na mshikamano hasa na maskini kwani hawa ni amana na utajiri wa Kanisa. Injili ya upendo, iwawezeshe watawa kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini, wakimbizi na wahamiaji; daima wakiendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Changamoto mbali mbali ziliwezeshe Kanisa kutoka ili kushuhudia huruma ya Mungu inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu. Baba Mtakatifu anawataka hata watawa kutoka tayari kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.