2017-02-10 15:24:00

Somalia imeandika ukurasa mpya wa demokrasia nchini humo!


Jumuiya ya Kimataifa inawapongeza Wabunge wa Somalia kwa kufanya uamuzi wa busara na hatimaye, kumchagua Bwana Mohamed Abdullahi Farmajo kuwa Rais wa Somalia, hatua kubwa kuelekea kwenye ujenzi wa demokrasia ya kweli nchini Somalia. Tarehe 8 Februari 2017 itakumbukwa na wananchi wengi wa Somalia kwa nchi yao kuandika ukurasa mpya katika mchakato wa demokrasia. Jambo la kutia moyo ni kuona kwamba hata Bwana Hassan Sheikh Mohamoud, Rais aliyemaliza muda wake wa uongozi alikubali matokeo na hivyo kurahisisha mchakato wa kipindi cha mpito katika kukabidhiana madaraka!

Wachunguzi wa mambo wanasema, Rais Mohamed Abdullahi Farmajo anakabiliwa na changomoto nyingi mbele yake, zinazohitaji umoja na mshikamano wa kitaifa ili kuweza kuzipatia ufumbuzi wa kudumu. Somalia inapaswa sasa kuanza mchakato wa misingi ya haki, amani na upatanisho wa kitaifa sanjari na usalama wa raia na mali zao kwani wananchi wa Somalia wamegawanyika na kusambaratika kutokana na sababu mbali mbali.

Rais mpya atapaswa kuimarisha miundo mbinu ya kiserikali; kusimama kidete kupambana na vitendo vya kigaidi vinavyoendelea kupandikiza hofu, mashaka na kifo miongoni mwa watu, pamoja na kuweka sera na mikakati itakayowawezesha mamilioni ya wakimbizi na wahamiaji kuweza kurejea tena nchini mwao, ili kuendelea na ujenzi wa nchi yao! Hapa pia Jumauiya ya Kimataifa itabidi kuunga mkono juhudi za Somalia katika ujenzi nchi hii ambayo kwa miaka mingi imekuwa ni uwanja wa vita!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.