2017-02-10 15:10:00

Mbinu mkakati wa kupambana na biashara haramu ya viungo vya binadamu


Taasisi ya Kipapa ya Sayansi imehitimisha mkutano wa kimataifa uliodumu kwa muda wa siku mbili yaani kuanzia tarehe 7- 8 Februari 2017 kuhusu mifumo mipya ya utumwa mamboleo, hususan biashara haramu ya viungo vya binadamu pamoja na wajumbe kutoa mapendekezo kumi na moja yatakayosaidia kupambana na biashara haramu ya viungo vya binadamu duniani! Haya ni mapendekezo ambayo yanapaswa kutekelezwa mara moja na serikali, vyombo vya sheria kitaifa na kimataifa ili kudhibiti biashara hii haramu inayoendelea kukua na kupanuka kila kukicha!

Jambo la msingi ni watu wa tamaduni na mataifa mbali mbali kutambua uwepo wa biashara haramu ya viungo vya binadamu vinavyoweza kunyofolewa kutoka kwa wafungwa magerezani, kwa njia ya malipo au hata kwa baadhi ya watu kujitolea viungo vyao; au ndugu na jamaa wa karibu kuamua kuuza viungo vya ndugu yao marehemu kuwa ni biashara inayopaswa kulaaniwa na wote! Viongozi wa kidini wasaidie kuwahamasisha waamini wao kujitolea baadhi ya viungo vya kwa ajili ya huduma ya upendo na mshikamano kwa wale wanaohitaji zaidi, kwa kuzingatia sheria, kanuni na maadili.

Wajumbe wa mkutano huu, wanashauri kuwepo na mbinu mkakati utakaosaidia kupata mahitaji msingi katika ngazi ya kitaifa na kimataifa; kwa njia ya ushirikiano na mshikamano wa kimataifa, ili upandikizaji wa viungo lisiwe ni jambo la dharura, bali sehemu ya mchakato unaoweza kufikiwa na wote. Vyombo vya ulinzi na usalama viandae sheria na kanuni zinazopaswa kufuatwa ili wale wanaovunja sheria hizi wafikishwe mbele ya sheria. Jambo hili linawezekana kwa kuridhia mikataba ya kimataifa na kikanda dhidi ya biashara haramu ya viungo vya binadamu.

Wahudumu wa sekta ya afya wanapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya kazi kwa kutambua madhara wanayoweza kupata wanaotoa au kupokea viungo vya wengine. Kuna haja pia ya kuanzisha mfumo wa mahakama utakaoshughulikia kesi za biashara haramu ya viungo vya binadamu katika maeneo husika pamoja na kushirikishana takwimu hizi na Jumuiya ya Kimataifa ili kuweza kudhibiti kuenea kwa biashara haramu ya binadamu.

Vyombo vya sheria vishirikiane kwa karibu sana na wafanyakazi katika sekta ya afya ili kubaini na hatimaye kuwafikisha watuhumiwa kwenye vyombo vya sheria, baada ya uchunguzi wa kina. Viongozi wahusika, Bima za Afya na Taasisi za huduma ziwe makini kwa kutojihusisha kulipia gharama za upandikizaji wa viungo au biashara haramu ya binadamu! Wafanyakazi katika sekta ya afya wanaojihusisha na masuala ya upandikizaji wa viungo vya binadamu wasaidie kuragibisha uelewa, sheria pamoja na miongozo ya kitaifa na kimataifa dhidi ya biashara haramu ya viungo vya binadamu. Mwishoni, wajumbe wanasema, Umoja wa Mataifa pamoja na Mashirika yake yanayopambana na matumizi haramu ya dawa za kulevya pamoja na uhalifu yashirikishane takwimu mintarafu upandikizaji wa viungo vya binadamu; kwa kuzingatia ukweli na uwazi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.