2017-02-08 15:18:00

Vijana changamkieni wito wa kipadre na maisha ya kitawa! Inalipa!


Kwa njia ya nadhiri ya usafi kamili, ufukara na utii, watawa wanakuwa ni mashuhuda na vyombo vya kinabii; chachu ya ujenzi wa misingi ya haki, amani, upendo na maridhiano kati ya watu! Hawa ni mashuhuda wa maisha ya kijumuiya chachu ya upendo, umoja na mshikamano, licha ya tofauti za kitamaduni, mahali anapotoka mtu na utaifa; changamoto zinazopaswa kufanyiwa kazi, ili kujenga udugu na mshikamano wa dhati kati ya watawa.

Haya ni maisha yanayoboreshwa kila siku kwa njia ya tafakari ya Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa, hususan Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Upatanisho ili kuambata huruma na upendo wa Mungu katika maisha. Kimsingi watawa ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake, maisha ambayo leo hii yanakabiliwa na changamoto za ubinafsi na hali ya kutaka kumezwa na malimwengu, mambo ambayo yanapaswa kuvaliwa njuga kwa kujikita katika majiundo makini awali na endelevu kwa watawa sanjari na kuambata mashauri ya Kiinjili kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani!

Askofu Evaristo Marcus Chengula wa Jimbo Katoliki Mbeya, hivi karibuni ameadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 20 tangu alipowekwa wakfu kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Mbeya, tayari kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu Jimboni Mbeya. Maadhimisho haya yamekwenda sanjari na Siku kuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni, ambayo pia ilikuwa ni Siku ya 21 ya Watawa Duniani kwa Mwaka 2017. Askofu Chengula ametumia nafasi hii kuwaalika vijana kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake katika maisha ya kitawa, tayari kuwapelekea watu wa Mungu Habari Njema ya Wokovu pamoja na huduma makini: kiroho na kimwili!

Itakumbukwa kwamba, Askofu Chengula ni Mtawa wa Shirika la Wamissionari wa Consolata, amechukua nafasi hii kuwaomba vijana kujitosa kimasomaso kwa ajili ya kujiunga na Shirika la Waconsolata, tayari kuwa ni vyombo vya faraja ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia, baada ya kufundwa kwa kina na mapana pale Morogoro, Tanzania na Kenya na baadaye kupelekwa Italia kwa ajili ya kupata masomo ya juu zaidi. Watawa wanapaswa kujenga maisha na utume wao kumzunguka Yesu wa Ekaristi kwa Ibada ya Misa Takatifu na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu mahali wanapojichotea nguvu, ari na maisha ya kitume, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza ili kuwa kweli ni Ekaristi inayomegwa kwa ajili ya huduma kwa familia ya Mungu. Watawa ni wachapa kazi, wanaotumwa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya maisha na huduma yao sehemu mbali mbali za dunia kwa kujenga na kudumisha ari na moyo wa kimissionari, kwani wanaitwa na kutumwa na Yesu Kristo Mfufuka ili kuwa kweli ni majembe yake yenye mvuto na mashiko!

Askofu Chengula ametumia fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza watawa kutoka mashirika mbali mbali ya kitawa na kazi za kitume yanayotekeleza utume wake kwa familia ya Mungu, Jimbo Katoliki Mbeya! Amewataka wazazi kuwaruhusu vijana wao ili waweze kujisadaka kwa ajili ya Mungu na jirani zao katika maisha ya wakfu! Ili kutekeleza dhamana hii, familia zinapaswa kuwa kweli ni shule ya miito, chemchemi ya maisha ya sala, utakatifu, upendo, huruma na msamaha wa kweli!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.