2017-02-08 15:01:00

Biashara haramu ya viungo vya binadamu duniani!


Utalii wa biashara haramu ya viungo vya binadamu una madhara makubwa katika maisha ya binadamu kwani una dhalilisha utu na heshima ya binadamu kiasi kwamba, binadamu anageuzwa kuwa kama bidhaa inayouzwa na kununuliwa sokoni! Vitendo hivi ni kinyume cha haki msingi za binadamu. Ni maneno yaliyotolewa na Askofu Marcelo Sanchèz Sorondo, Mkuu wa Taasisi ya Kipapa ya Sayansi, Jumanne, tarehe 7 Februari 2017 wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kimataifa kuhusu mifumo mipya ya utumwa mamboleo, hususan biashara ya viungo vya binadamu!

Wajumbe wamepata nafasi ya kusikiliza kwa makini yaliyomo kwenye nyaraka mbili muhimu mintarafu biashara haramu ya viungo vya binadamu yaani: Tamko la Istanbul la Mwaka 2008 pamoja na Waraka kuhusu Mabadiliko ya Biashara Haramu ya Binadamu uliotolewa na Baraza la Jumuiya ya Ulaya kunako mwaka 2014. Tamko la Istanbul linakazia pamoja na mambo mengine umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kuzingatia sheria, maadili na weledi katika mchakato wa kudhibiti shughuli za utoaji wa viungo vya binadamu pamoja na wahusika kuhakikishiwa usalama wa maisha yao mintarafu miiko na maadili ya kazi.

Tamko hili linakaza kusema, uvunjwaji wa kanuni maadili ni matokeo ya hitaji kubwa la watu wanaohitaji kupatiwa viungo sehemu mbali mbali za dunia, kiasi cha kuwafanya wafanyakazi katika sekta hii kupata kishawishi cha kujingiza kwenye biashara haramu ya viungo vya binadamu. Changamoto kwa nchi husika ni kuhakikisha kwamba zinajitahidi kukidhi mahitaji ya wagonjwa wake kwa kuzingatia sheria za kitaifa na kimataifa sanjari na sera zilizobainishwa.

Waraka kuhusu Mabadiliko ya Biashara Haramu ya Binadamu uliotolewa na Baraza la Jumuiya ya Ulaya unalenga pamoja na mambo mengine kudhibiti biashara haramu ya viungo vya binadamu kwa kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wahusika wote; kuwalinda wahanga wa biashara hii haramu pamoja na kukoleza ushirikiano katika ngazi ya kitaifa na kimataifa mintarafu uwajibikaji katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu. Wajumbe, wamepata nafasi ya kusikiliza madhara ya biashara haramu ya viungo vya binadamu kutoka Canada, Marekani, Mexico, Guatemala, Perù, Costa Ricca, Nicaragua, Colombia, Argentina na Brazil. Wajumbe  pia wamebahatika kusikiliza shuhuda za biashara haramu ya viungo vya binadamu kutoka Barani Afrika hasa katika nchi za Misri, Nigeria, Lybia, Sudan, Eritrea na Somalia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.