2017-02-07 13:52:00

Mabalozi tafuteni wawekezaji kwa ajili ya Tanzania!


Waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amewataka Mabalozi wa Tanzania katika nchi mbalimbali kuhakikisha wanatumia uwakilishi wao kutafuta wawekezaji watakaokwenda kuwekeza katika sekta ya viwanda nchini Tanzania. Amesema mkakati wa Serikali awamu ya tano ni kuimarisha uchumi hadi wa kati kupitia sekta ya viwanda, hivyo jukumu la mabalozi hao ni kuhakikisha jambo hilo linafanikiwa.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo Jumanne, Februari 7, 2017 alipokutana na Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi za Uturuki, Brazil, China, Italia, Ufaransa, Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Uswisi. Mabalozi hao ni Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi (Brazil), Balozi Elizabeth Kiondo (Uturuki), Balozi George Madafa (Italia), Balozi James Msekela (Uswisi), Balozi Samuel Shelukindo (Ufaransa), Balozi Paul Mella (DRC), Balozi Mbelwa Kairuki (China). “Serikali inahitaji watu wa kuja kuwekeza katika viwanda ili kuongeza thamani ya mazao kabla ya kuyauza nje ya nchi, hivyo jukumu lenu ni kuhakikisha tunapata wawekezaji wenye sifa,” amesema.

Pia Waziri Mkuu amewataka mabalozi hao kutumia uwakilishi wao katika nchi hizo kwa kuhakikisha wanatangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini ili kuongeza idadi ya watalii wanaokuja Tanzania.  Aidha, Waziri Mkuu amewataka mabalozi hao kulinda maslahi ya Taifa katika nchi hizo ikiwa ni pamoja na kuimarisha uhusiano uliopo kati ya Tanzania na mataifa hayo.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka mabalozi hao kuhakikisha wanawatambua Watanzania wanaoishi katika mataifa hayo na kushirikiana nao katika kutafuta wawekezaji wa kuja kuwekeza nchini Tanzania Kwa upande wake Balozi Paul Mella (DRC) ambaye alizungumza kwa niaba ya Mabalozi wenzake alimuhakikishia Waziri Mkuu kwamba watakwenda kutekeleza wajibu wao ipasavyo.

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU. 








All the contents on this site are copyrighted ©.