2017-02-06 09:08:00

Maadhimisho ya Siku ya 39 ya Uhai Kitaifa nchini Italia!


Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, Jumapili tarehe 5 Februari 2017 limeadhimisha Siku ya 39 ya Maisha Kitaifa kwa kuongozwa na kauli mbiu “Wanawake na wanaume kwa ajili ya maisha kwa kuiga mfano wa Mama Theresa wa Calcutta”. Askofu msaidizi Lorenzo Leuzzi wa Jimbo kuu la Roma, ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa la “Santa Maria in Trasportina” na baadaye yakafuatia maandamano makubwa kwa ajili ya kuenzi Injili ya uhai kuelekea kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwa ajili ya kusali Sala ya Malaika wa Bwana pamoja na Baba Mtakatifu Francisko.

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia katika ujumbe wake kwa maadhimisho haya linaialika familia ya Mungu nchini Italia kuwa na ujasiri wa kuota ndoto pamoja na Mwenyezi Mungu, ili kuweza kuthubutu kufanya maamuzi magumu katika maisha, kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Yosefu mtu wa haki. Hata leo hii, kuna umati mkubwa wa waamini wanaoendelea kutekeleza ndoto ya maisha katika familia, kwa kujitahidi kujenga na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu ambaye daima anafanya hija pamoja na waja wake.

Baba Mtakatifu anasema, kuota ndoto pamoja na Mwenyezi Mungu kunamwilishwa katika historia kwa kuwatunza na kuwaenzi watoto na wazee, kwani hawa ni tumaini la leo na kesho iliyo bora zaidi; wazee wana kumbu kumbu hai ya tunu msingi za kifamilia; ni watu waliothubutu kurithisha imani, upendo na matumaini kwa siku za usoni, kwani ndoto yao inajikita katika nguvu na kumbu kumbu hai ya kuweza kusonga mbele. Ili kuweza kufanikisha azma ya kuwatunza watoto na wazee, kuna haja ya kuwa na sera za uchumi unaowajibika dhidi ya utamaduni wa kifo.

Hapa kuna haja ya kusimama kidete kuelimisha, kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai, ili kuganga na kuponya utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine; utamaduni wa ubinafsi unaoendelea kusababisha idadi ya watoto wanaozaliwa nchini Italia kushuka kila mwaka. Ni changamoto ya kusimama kidete kupambana na sera zinazosambaza utamaduni wa kifo kwa kukumbatia utoaji mimba na kifo laini! Mama Theresa wa Calcutta ni mfano bora wa kuigwa katika kukabiliana na changamoto dhidi ya utamaduni wa kifo, kwa kusimama kidete kujenga na kudumisha Injili ya uhai inayothamini maisha tangu pale mtoto anapotungwa mimba hadi mauti yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu.

Huu ni mwaliko wa kuendelea kuimba utenzi wa sifa na shukrani kuhusu: uzuri na utakatifu wa maisha kwani hii ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayopaswa kulindwa, kudumishwa na kuendelezwa. Maisha ni fursa inayopaswa kuchangamkiwa na wengi; ni heri inayotakiwa kumwilishwa, ni ndoto inayopaswa kuwa ni uhalia wa maisha; maisha ni Injili inayopaswa kutangazwa na kushuhudiwa! Mama Theresa wa Calcutta anawafundisha watu kusikiliza na kujibu kilio cha Yesu Msalabani! Nina kiu! Hiki ni kilio ambacho kimejificha miongoni mwa watoto wadogo ambao hawajabahatika hata kuuona mwanga wa jua la maisha ya duniani. Hawa ni maskini wanaohitaji amani inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, Mwana Kondoo wa Mungu, aliyechinjwa, lakini akawa ni mshindi dhidi ya dhambi na mauti! Yesu ni mto na chemchemi ya maisha mapya, chanzo cha ujasiri wa watu wanaothubutu kusimama kidete kulinda, kutetea na kushuhudia Injili ya uhai inayofumbatwa katika Injili ya familia; maisha na utume wa kipadre na kitawa.

Inapendeza wanasema Maaskofu Katoliki wa Italia, kuota ndoto na vijana wa kizazi kipya kwa ajili ya Kanisa na Taifa linalo enzi upendo ambao uko tayari kupokea na kulea Injili ya uhai, zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ni mwaliko wa kuthamini Injili ya uhai hata kwa wale wanaoteseka, wakimbizi na wahamiaji, mtindo wa maisha unaofumbatwa katika fadhila za Bikira Maria, aliyejitahidi kutekeleza mpango wa Mungu katika maisha yake. Watu wawe na ujasiri wa kujisadaka kwa ajili ya jirani zao ili kuambata upendo wa Mungu unaofariji, unaosaidia na kumwambata mwanadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.