2017-02-06 10:09:00

Askofu George Bugeja ateuliwa kuwa Askofu mpya wa Tripoli, Libya


Baba Mtakatifu Francisko ameridhia ombi lililowasilishwa kwake na Askofu Giovanni Innocenzo Martinelli wa Jimbo la Kitume la Tripoli, Libya la kung’atuka kutoka madarakani. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu George Bugeja, O.F.M kuwa Askofu mpya wa Jimbo la Kitume la Tripoli. Kabla ya uteuzi huu, Askofu Bugeja alikuwa ni Askofu mwandamizi wa Jimbo la Kitume la Tripoli, Libya, sehemu ambayo kwa sasa inakabiliwa na changamoto nyingi katika maisha na utume wa Kanisa.

Itakumbukwa kwamba, Askofu George Bugeja alizaliwa kunako tarehe 1 julai 1962. Baada ya masomo na majiundo yake ya kitawa katika Shirika la Ndugu Wafranciskani Wakapuchini, O.F.M. aliweka nadhiri zake za daima kunako tarehe 28 Agosti 1983. Tarehe 10 Julai 2015 akateuliwa kuwa Askofu mwandamizi wa Jimbo la Kitume la Tripoli, nchini Libya na kuwekwa wakfu hapo tarehe 4 Septemba 2015. Tarehe 14 Februari 2016 akateuliwa kuwa ni Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki Benghazi, Libya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.