2017-02-04 09:35:00

Papa Francisko: Colombia jengeni madaraja ya amani na upatanisho!


Mkutano wa XVI wa Kimataifa wa Tuzo ya Amani Duniani umefunguliwa huko Bogotà, Colombia kuanzia tarehe 2 Februari na unafungwa rasmi tarehe 5 Februari 2017. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa wajumbe hawa anasema anapenda kutoa salam na matashi mema kwa washiriki wote wa mkutano huu. Baba Mtakatifu anapenda kuwatia shime wajumbe wa mkutano kujizatiti zaidi katika mchakato wa uelewano na majadiliano kati ya watu wa mataifa.

Baba Mtakatifu anapenda kuihamasisha Colombia kuwa mstari wa mbele katika ujenzi wa daraja la amani na upatanisho; mambo msingi yanayoweza kuwasaidia watu kuishi kwa amani na kuvuka kinzani na mipasuko ya kijamii. Baba Mtakatifu anawataka wananchi kushinda kishawishi cha kutaka kulipiza kisasi na matokeo yake, wawe ni mashuhuda na wajenzi wa amani duniani. Anawataka kukataa katu katu kutumia faslafa ya mtutu wa bunduki na badala yake wajitahidi kukuza na kujenga utamaduni wa amani unaofumbatwa katika mahusiano, maamuzi na matendo yao katika medani mbali mbali za maisha. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anawaombea Baraka, hekima na nguvu wajumbe wote wa Mkutano huu. Ujumbe huu umewasilishwa kwenye mkutano huu na Askofu mkuu Ettore Balestrero, Balozi wa Vatican nchini Colombia

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.