2017-02-04 15:07:00

Mapambano dhidi ya baa la umaskini duniani!


Chama cha Kitume cha Wafokolari kuanzia tarehe 1- 5 Februari 2017 kimekuwa kikiendesha mkutano kuhusu dhana ya uchumi na umoja kwa kuwashirikisha wajumbe 1, 100 kutoka katika nchi 49 duniani. Kutoka Barani Afrika, wajumbe walioshiriki ni wale wanaotoka Burkina Faso, Burundi, Cameroon, Pwani ya Pembe, Ethiopia, Nigeria, DRC na Uganda. Mkutano huu umekuwa ukifanyika huko mjini Castel Gandolfo, nje kidogo na mji wa Roma. Tarehe 4 Februari 2017 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtaktifu Francisko mjini Vatican.

Lengo la mkutano huu ni kuendeleza mchakato wa mapambano dhidi ya baa la umaskini duniani. Takwimu zinaonesha kwamba, ni watu 8 peke yao wanaomiliki nusu ya utajiri wa dunia hii, wakati kuna mamilioni ya watu wanaoendelea kutumbukia katika baa la umaskini wa hali na kipato. Matokeo yake ni kuendelea kupanuka kwa pengo kati ya matajiri na maskini akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi. Kuna haja ya kubadili mfumo wa uchumi duniani kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na mahitaji msingi ya binadamu. Lengo ni kuibua sera na mikakati ya uchumi shirikishi, tayari kupambana na umaskini duniani.

Kunako mwaka 1991 Chiara Lubich akiguswa na umaskini huko nchini Brazil, aliamua kuwashirikisha wafanyabiashara kuchangia kwa hali na mali katika mchakato wa kupambana na umaskini wa hali na kipato duniani. Rasilimali fedha iliyopatikana imesaidia kwa kiasi kikubwa kupambana na umaskini miongoni mwa familia nyingi sehemu mbali mbali za dunia. Fedha imechangia kukuza na kuibua fursa za ajira hasa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya. Changamoto hii imekuwa ni nafasi ya kuendeleza utamaduni wa kutoa kuliko kupokea.

Wajumbe hawa ambao wengi wao ni wanafunzi, vijana, wasomi pamoja na maprofessa ambao kwa njia ya mtandao wa kijamii wanataka kuanzisha nadharia ya uchumi wa umoja kwa njia ya mitandao ya kijamii. Wanakusanya sera na mikakati mbali mbali ili kupambana na baa la umaskini duniani pamoja na kuangalia kwa umoja hali ya umaskini duniani, kuguswa na hatimaye kusikiliza kilio na kujibu kilio cha maskini. Lengo ni kushikakama kwa dhati kabisa katika mapambano dhidi ya umaskini duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.