2017-02-04 14:49:00

Jengeni uchumi shikamanishi ili kupambana na umaskini!


Dhana ya uchumi na umoja; rasilimali fedha; baa la umaskini duniani na matumaini ya ukuaji wa uchumi katika mshikamano, ili kuboresha kiwango na ubora wa uzalishaji wa bidhaa na huduma kwa binadamu! Haya ni mambo msingi yaliyochambuliwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 4 Februari 2017 alipokutana na kuzungumza na wajumbe waliokuwa wanashiriki katika mkutano wa kiuchumi ulioandaliwa na Chama cha Kitume cha Wafokolari. Dhana ya uchumi na umoja ilianzishwa na Chiara Lubich miaka 25 iliyopita ili kukabiliana na changamoto ya umaskini duniani kwa kujikita katika kipaji cha ugunduzi, huku wakiendelea kuwa ni vyombo na mashuhuda wa umoja.

Dhana hii ikaleta mabadiliko makubwa katika mfumo wa watu kuishi na kutenda katika umoja na mshikamano wa dhati. Baba Mtakatifu anakazia umoja na mshikamano wa maisha ya kiroho unaoweza kufumbata na kuboresha umoja wa rasilimali vitu, karama na faida za kiuchumi. Rasilimali fedha ni kiini cha umoja na mshikamano katika uchumi. Lakini rasilimali fedha isiwafanye watu kuwa ni watumwa dhana iliyopingwa na Kristo Yesu kwa nguvu zote. Rasilimali fedha iwe ni nyenzo inayowawezesha watu kujipatia mahitaji yao msingi.

Uchu wa fedha na mali ni dhambi kwani humfanya mwanadamu kujiamini kupindukia na kuanza kujitafuta mwenyewe katika ubinafsi wake na matokeo yake ni madhara makubwa katika mafungamano ya kijamii. Uchu wa fedha umepelekea watu wengi kujitumbukiza katika michezo ya kamari na matokeo ni kusambaratisha familia sehemu mbali mbali za dunia. Fedha “eti ni sababuni ya roho”, lakini kwa sasa imegeuka kuwa ni fedheha kwani inamtumbukiza mwanadamu katika ulaji wa kupindukia. Kumbe, hapa kuna haja ya kujikita katika tunu msingi za maisha ya kiroho kwa kutumia faida inayopatikana kutokana na rasilimali fedha kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kwa njia hii, Chama cha Kitume cha Wafokolari kimeshinda kushawishi cha uchu wa fedha na mali, kwani rasilimali fedha inatumika kwa ajili kukuza na kudumisha mshikamano na wala haigeuzwi kuw ni mungu mdogo!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, wakati huu kuna mwamko mkubwa wa kupambana na baa la umaskini duniani; watu ambao kwenye Maandiko Matakatifu walikuwa na nafasi ya pekee ya kupewa misaada, lakini misaada hii haikufua dafu, kiasi cha kujikuta wakiwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Leo huu, kuna mashirika na miundo mbinu mbali mbali inayojikita katika mapambano dhidi ya baa la umaskini duniani. Ukusanyaji wa kodi unapania kujenga mshikamano na kusaidiana kwa hali na mali. Lakini kwa bahati mbaya ubepari unaendelea kuzalisha makundi makubwa ya maskini wanaosukumizwa pembezoni mwa jami na hatimaye, kufichwa ili yasionekane.

Ni kiasi kidogo tu cha faida kubwa inayopatikana katika uzalishaji na huduma kinatumika katika kusaidia kugharamia huduma za kijami. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, huduma hii itaweza kufikia kilele chake pale wafanyabiashara wa silaha duniani watakapoanza kutumia faida yao kwa ajili ya kutibu wagonjwa hospitalini pamoja na kuwasaidia walemevu waliokatika viungo kwa sababu ya mabomu. Kumbe, uchumi wa mshikamano ili kuendelea kuwa aminifu kwa karama yake, lazima kusitisha kabisa utengenezaji na ulimbikizaji wa silaha ambazo ni chanzo magonjwa na ulemavu kwa mamilioni ya watu duniani.

Kutakuwepo na sherehe ya uchumi wa umoja ikiwa kama maskini watapungua na hatimaye kutoweka kutoka katika uso wa dunia. Haitoshi kwa wafanyabiashara kuwa ni wasamaria wema, bali wanapaswa pia kushirikisha mchakato mzima wa soko la bidhaa zinazozaliwashwa au huduma inayotolewa, kabla ya watu kuanza kuwa majambazi. Mfano wa Baba mwenye huruma unapaswa kuigwa hapa: kwa kusamehe na kusahau; kufadhili na kuokoa maisha na utu wa watu. Hakuna mtu anayepaswa kufa kwa baa la njaa na utupu duniani.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, katika kipindi cha miaka 25 Wafokolari wameshuhudia kwamba, kuna uwezekano mkubwa wa kujenga uchumi wa mshikamano, kwa kukaa na kukua kwa pamoja, hali ambayo kwa sasa inakabiliwa na changomoto kubwa. Lakini, wakiwa waaminifu hata katika udogo wao wanaweza bado wakaishi na kukuwa huku wakiwa wameshikamana kwa kuzalisha kwa wingi pamoja na kuzingatia ubora, ili kuokoa maisha ya maskini duniani.

Chachu ya mshikamano ni muhimu sana katika kuleta mageuzi kwa maisha ya watu. Huu ni mwaliko wa kuwa ni chachu ili kuyachachua malimwengu kwa kushikamana na maskini pamoja na vijana wa kizazi kipya; kwa kujifunza kujitoa wenyewe pamoja na kuwashirikisha wengine faida yao. Rasilimali fedha isaidie kuokoa maisha ya maskini na vijana wa kizazi kipya wanaohitaji majibu yanayofumbatwa katika udugu wenye heshima na unyenyekevu. Ukarimu wa watu iwe ni chachu ya upendo, udugu na mshikamano wa dhati. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawataka wajumbe wa Fokolari kuguswa na mahangaiko ya maskini. Kutumia faida ya rasilimali fedha kupambana na uchu wa fedha na mali. Ni mchakato wa kusaidia kupambana na uchumi unaoendelea kuwatumbukiza watu katika majanga mbali mbali ya maisha. Anawatakia mema katika maisha na utume wao, ili waendelee kuwa na ujasiri, unyenyekevu na furaha, kwani Mungu anawapenda wake wanaijisadaka bila ya kujibakiza.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.