2017-02-03 08:30:00

Yesu apewe kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wa watawa!


Baba Mtakatifu Francisko, katika maadhimisho ya Siku kuu ya kutolewa Bwana Hekaluni, sanjari na Siku ya 21 ya Watawa Duniani, Alhamisi, tarehe 2 Februari 2017 ameongoza maandamano ya watawa waliokuwa wamebeba mishumaa inayowaka na baadaye kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu katika mahubiri yake ametafakari kuhusu wimbo wa Simeoni aliyebahatika kuuona wokovu wa Mungu aliokuwa ameuweka tayari machoni pa watu wake Israeli sanjari na kukumbatia matumaini, yaliyomjaza furaha kwa kuona kwamba, Mwenyezi Mungu anaishi kati pamoja na watu wake na hivyo kuwa ni sehemu ya maisha yao!

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwamba, wazazi wa Mtoto Yesu walikuwa wanatekeleza sheria kwani zilipotimia siku za kutakasika kwao, Mtoto Yesu alitolewa Hekaluni, nafasi ya kukutana na watu wake waliokuwa wanamsubiri kwa njia ya imani, kiasi kwamba, tukio hili likawa ni chemchemi ya furaha na upyaisho wa matumaini. Wimbo wa Simeoni ni wimbo wa mwamini anayethubutu kusema kwa uhakika kwamba, matumaini kwa Mwenyezi Mungu kamwe hayawezi kudanganya.

Simeoni na Anna ni mashuhuda wanaomtukuza na kumwimbia Mungu juu ya zawadi ya maisha inayopaswa kufumbatwa katika matumaini kwani Mwenyezi Mungu ambaye daima anatekeleza ahadi zake kama ambavyo Kristo Yesu atakavyofafanua mwenyewe katika sinagogi la Nazareti kwa kusema kwamba: Roho wa Bwana yu juu yake kwani ametumwa kuwatangazia Habari Njema: wagonjwa, wafungwa, wapweke, maskini, wazee pamoja na wadhambi ambao pia wanapaswa kumwimbia Mungu utenzi wa matumaini, kwani Yesu yuko pamoja nao na anaendelea kuwa pamoja na waja wake!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, wimbo wa matumaini ni urithi kutoka kwa Mababu wa imani unaofumbata nyuso, maisha pamoja na majitoleo yanayomwilishwa kila siku ya maisha yao. Waamini pia ni warithi wa ndoto na imani ya Mababu zao ambayo kamwe haiwezi kudanganya! Ni warithi wa ujasiri wa ndoto ya wazee inayowawezesha hata leo hii waamini kuweza kuimba kwa kusema, kweli Mwenyezi Mungu ni mwaminifu na matumaini kwake hayawezi kumdanganya mtu kwani Mungu anawatembelea watu wake. Waamini wa nyakati hizi nao pia wamebahatika kupata Roho wa Bwana na hivyo kuwa ni manabii wenye ndoto na maono, ili kuiendeleza ndoto hii.

Baba Mtakatifu amewakumbusha watawa kwamba kwa kufumbata ndoto na maono haya wataweza kuepuka kishawishi cha kuwa “wagumba” katika maisha ya kitawa; yaani kuwa na maisha ya kujikimu peke yake. Kishawishi hiki kitawafanya watawa kujifungia katika ubinafsi, majumba na miundo mbinu yao, kiasi hata cha kuwarudisha nyuma kabisa badala ya kuwapeleka mbele kuendeleza kipaji cha ugunduzi wa kinabii unaofumbatwa katika ndoto ya waanzilishi wa mashirika yao. Kwa mtindo huu wa maisha anasema Baba Mtakatifu, watawa watajikuta wakitafuta njia ya mkato katika maisha ili kukimbia mbali na changamoto za ulimwengu mamboleo zinazoendelea kubisha hodi katika malango ya maisha yao.

Saikolojia ya maisha ya kujikimu inawaondolea watawa nguvu na kipaji cha ugunduzi kiasi hata cha kushindwa kuanzisha mchakato utakaowawezesha kusonga mbele; inawafanya kusahau neema ya maisha ya kitawa kiasi cha kuwageuza kuwa ni “watu wa mshahara” badala ya kuwa ni watu wa matumaini wanaoitwa na kutumwa kushuhudia unabii kama fursa ya utume wao, changamoto na mwaliko kwa watawa kuwa macho na makini ili kamwe wasitumbukie katika hali hii ya maisha!

Mzee Simeoni na Anna ni mashuhuda wa imani ambao hawakubaki wamejifungia katika ubinafsi, wasi wasi wala woga wa mabaya yanayoweza kuwafika katika uzee wao, bali walikuwa ni watu wa matumaini yaliyotua nanga kwa kukutana na Kristo Yesu, kiasi cha Mzee Simeoni kuimba utenzi wa sifa na shukrani unaoshuhudia ndoto yake ya imani. Yesu anakuwa ni chemchemi ya furaha na matumaini katika maisha yake, mwelekeo mpya wa kuondokana na maisha ya kujikimu, tayari kuanza mchakato wa maisha mapya kwa kumpatia nafasi Yesu ya kuweza kuwa kati pamoja na watu wake.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, ulimwengu mamboleo unaendelea kukumbana na mabadiliko makubwa, kumbe ni wajibu wa watawa kumweka Kristo kuwa ni kiini cha mabadiliko haya kwa njia ya karama za mashirika zinazomwilishwa katika uhalisia wa maisha kwa kuyachachua malimwengu, kiasi kwamba, ile mbegu njema iiliyopandwa katika nyoyo za watu iweze kukua na kukomaa licha ya magugu yanayoizingira. Watawa wanapaswa kuwa ni watu wa tafakari, ili kumwezesha Yesu kuwa kati pamoja na watu wake, ili kung’amua jinsi ambavyo Mungu anafanya hija na waja wake.

Uwepo wa Kristo kati ya watu wake, uwawezeshe watawa kubeba Misalaba ya ndugu zake Kristo, kwa kugusa na kuganga madonda ya Kristo yanayojionesha kati ya ndugu zake maskini na wadogo sehemu mbali mbali za dunia. Yesu apewe nafasi ya pekee kati pamoja na watu kwa kutambua kwamba, wanaendelea kusamehewa dhambi zao na kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo inayowaunganisha na waamini wengine, wamepakwa mafuta ili kuwa faraja ya Mungu kwa jirani zao. Yesu akiwa kati yao, watakuwa na uwezo wa kuishi na kushikamana kiasi hata cha kuonja mang’amuzi ya hija ya maisha ya mshikamano na udugu, chachu ya matumaini  na wimbo mpya. Hili linawezekana kwa kugeuza ndoto ya wazee wa imani kuwa ni unabii. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawataka watawa kumweka Kristo kuwa ni kiini cha maisha na vipaumbele vya watu wake si kwa kulalama, bali katika wimbo, amani na utulivu; kwa kumtumainia na kujiaminisha kwa Roho Mtakatifu, kwani huu ni wimbo unaochipua matumaini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.