2017-02-03 12:21:00

Matendo yenu mema yawe ni ushuhuda wenye mvuto na mashiko!


Palitokea miaka kadhaa iliyopita nchini Tanzania tangazo moja la biashara juu ya bidhaa ya soda aina ya “Krest – Bitter Lemon”. Tangazo hili lilionesha kundi la watu ambao hawakutambulika vizuri wakimzunguka msichana mrembo ambaye anaonekana vizuri huku wakimshangaa kwa sababu alikuwa anaitumia bidhaa hiyo. Chini yake yaliwekwa maneno yaliyobeba mahudhui ya tangazo hilo yakisomeka: “Stand out of the crowd”. Hii ilimaanisha kwamba yeye ambaye anatumia bidhaa hiyo alikuwa anajitokeza na kujitofautisha na wengine katika umati wa watu. Kamwe usingeweza kumsawazisha na watu wengine wanaomzinguka kwani bidhaa hiyo ilimtanabaisha na kumtenga na kundi hilo kwa utambulisho wake rasmi.

Injili ya Dominika hii inatukumbusha wajibu wetu wakristo wa kuwa kama bidhaa hiyo iliyotangazwa, yaani kuonesha utambulisho wetu katika jamii na si kusawazishwa na watu wengine; kufanya lile lililo tofauti na linalomtukuza Mungu katika jamii ya wanadamu. Kristo anatumia lugha ya picha ya chumvi na mwanga, vitu ambavyo uwepo wake katika mazingira yake ni dhahiri. Na hapo ndipo anapotutaka sisi Wakristo kujidhihirisha, kujitokeza kwa kuwa mwanga na chumvi katika jamii. Ni vema kutafakari matumizi ya chumvi na mwanga katika jamii ili kupata maana halisi ya Kristo.

Chumvi katika chakula ina kazi ya kuongeza ladha. Mmoja anapokionja chakula mara moja huisikia ladha lake na matokeo yake ni kukifurahia chakula. Kila mmoja hupenda chakula chenye ladha ya chumvi ndiyo maana ni aghalabu kukosekana kwa chumvi ya ziada mezani wakati wa kula ili mmoja anapoona haijakolea kadiri ya hitaji lake huongezea kidogo. Kristo anatuambia kwamba “chumvi ikiwa imeharibika itatiwa nini hata ikolee?” Chumvi ambayo inashindwa kutambulisha uchumvi wake haitofautiani na chumvi mawe ambayo badala ya kuyeyuka na kuchanganyika na chakula hubaki katika ugumu wake na kuharibu meno.

Mwanga husaidia kuondoa giza. Mmoja anapowasha taa anategemea itoe nuru na kumsaidia kuona vema gizani. Hivyo kazi ya mwanga inajidhihirisha pale mwanga huo unapoangaza na kusaidia kuonesha kile kilichofichika kwa sababu ya giza. Kristo anatuambia kwamba “watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kiango nayo yawaangaza wote”. Ni kihoja kwa mmoja kuwasha taa na kuiweka chini ya kitanda. Maana yake ni kihoja mmoja kujisikia kuwa yu mkristo lakini matendo yake hayadhihirishi ukristo wake au ni kihoja kuonekana mtu wa ibada na sadaka lakini maisha yako hayaakisi neema hiyo unayoipokea.

Maisha yetu ya kikristo yanarandanishwa na chumvi au mwanga. Jambo la pamoja tulionalo katika mifano hii ya chumvi na mwanga ili kuifunua hadhi yake na kujitambulisha mbele ya watu ni utayari wa kuteketea kwa ajili ya wengine. Chumvi isipoyeyuka haiwezi kutoa ladha hali kadhalika mafuta yasipoteketea au mshumaa kuyeyuka katu hautoi mwanga. Kama bidhaa hizi zingejitafuta kuonekana mbele ya watu zingepoteza ile hadhi ya kuonekana na kujitambulisha kiasi cha kuonekana hazifai kabisa. “Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni”. Nabii Isaya katika somo la kwanza anatuonesha namna iliyo njema ya kujiteketeza ili kutoa harufu nzuri ya matendo mema yanayomtumuza Mungu. Hili linaonekana katika matendo yetu ya ukarimu kwa jirani zetu. Nabii Isaya anatutanabaisha kwamba, unapowatendea wenzako mema “ndipo nuru yako itakapopambazuka kama asubuhi, na afya yako itatokea mara; na haki yako itakutangulia; utukufu wa Bwana utakufuata nyuma ukulinde”. Mema tunayoyatenda yanaifunua haiba yetu na yanatufanya tutambulike kuwa sisi wana wa Mungu. Muunganiko huo na wenzetu utaendelea kutupatia baraka kwa kuwa Bwana atakuwa pamoja nasi.

Moja ya misemo katika lugha ya Kiswahili unasema: “tenda wema nenda zako usingoje shukrani”. Tungo hii inarandana kabisa na mahusia ya kiinjili tunapoambiwa: “mtakapokwisha kuyafanya yote mliyoagizwa, semeni, ‘sisi tu watumwa wasio na faida; tumefanya tu yaliyotupasa kufanya” (Lk 17:10). Mara nyingi tunapowatendea mema wenzetu huwa tunasongwa na kishawishi cha kutafuta jina na umaarufu. Hatutafuti kumtukuza Mungu bali ni kujitukuza sisi. Tunaigeuza kazi njema tuifanyayo kama tangazo la biashara. Hapa huwa tunashindwa kujiyeyusha ili kutoa ladha nzuri au kuteketea ili kutoa mwanga na hivyo sifa yetu ya ukristo inachakachuliwa. Tujiulize! Ni mara ngapi tunataka kutenda wema fulani iwe ni matendo ya huruma huku tukisindikizwa na vyombo vya habari au umati wa watu wanaotupigia makofi? Mara ngapi tusipopewa shukrani tunaanza kulalama kwamba huyu uliyemfanyia wema hajali lile ulilomtendea? Nimeshawahi kushuhudia mmoja aliyefika kutoa msaada katika katika kituo cha watoto yatima akisitisha huduma hiyo kisa ni kutokuwepo kwa vyombo vya habari.

Mtume Paulo anatupatia nyenzo ya kutumia katika kutekeleza ukarimu wetu kama bendera ya ukristo wetu na tendo la kumtukuza Mungu. Hapa anaendelea kuugusia msalaba wa Kristo kuwa nyenzo na kielelezo ambapo tuukumbatiapo matendo yetu mema humtukuza Mungu Baba yetu wa mbinguni. Kristo ametufundisha juu ya msalaba maana ya kuyeyuka na kujiteketeza ili kutoa ladha na mwanga wa neema za Mungu kwa wengine. Kujionesha kwetu huku katika kumtukuza Mungu kunakuwa ni sababu ya mahusiano mema na wenzetu na njia ya kutufikisha katika kuthaminiana katika utu wetu. Tunachofundishwa juu ya msalaba ni kutanguliza utukufu wa Mungu, ni kuung’arisha utukufu wa Mungu kwa kuyatimiza mapenzi yake.

Ni fursa kwetu kutafakari namna ambavyo tunajitambulisha kama wakristo. Je, ninaicheza namna gani nafasi yangu niliyopangiwa na Mwenyezi Mungu? Je, katika familia yangu hakuna mafarakano sababu tu sijitambulishi kama baba anayepaswa kuilinda na kuitunza familia bali kama mtwana anayepaswa kutumikiwa na wengine? Au sijitambulishi kama mama anayepaswa kutoa malezi na upendo bali mshindani ninayetafuta ukubwa na umwamba ndani ya familia? Je, katika sehemu yangu ya kazi au biashara hakuonekani kuwa na ladha au mwanga sababu tu nimeweka mbele maslahi binafsi na hivyo uzembe, rushwa na ubadhirifu vinatawala hata kama vinawanyima wengine haki zao? Je, nafasi yangu kama kiongozi wa jamii inauangaza vipi utukufu wa Mungu?

Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.