2017-02-02 14:45:00

Mshikamano katika kulinda, kutetea na kudumisha utu wa binadamu


Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujizatiti zaidi katika kujenga na kudumisha Injili ya amani na usalama duniani kwa njia ya mshikamano unaofumbatwa katika kanuni auni, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwa kukataa kishawishi cha kutaka kujifungia katika ubinafsi. Biashara ya silaha ni tishio kwa amani na usalama wa Jumuiya ya Kimataifa. Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kukoleza mchakato wa majadiliano kati ya watu katika ukweli na uwazi, ili hatimaye, kujenga utamaduni na madaraja ya watu kukutana.

Hii ni changamoto na mwaliko wa kuwa na mwelekeo mpya na mpana zaidi ili kusimamia haki msingi za binadamu, haki na amani kwa wananchi wa Madagascar. Haya yamesemwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican wakati wa ziara yake ya kwanza Barani Afrika huko Madagascar, Jumanne tarehe 31 Januari 2017 kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Madagascar. Ujenzi wa madaraja ya watu kukutana na kujadiliana ni mchakato unaohitaji ujasiri na udumifu kwa kuondokana na ubinafsi, pamoja na utaifa usiokuwa na mashiko wala mvuto.

Kishawishi cha kutaka kujifungia katika ubinafsi kwa kisingizio cha ulinzi na usalama wa taifa; utamaduni, imani na ukuzaji wa sera na uchumi wa ndani ni hatari kwa mafungamano ya kimataifa anasema Kardinali Parolin. Kuna haja ya kusimama kidete kutetea utu na heshima ya binadamu hasa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; kwa kukuza na kudumisha utamaduni wa majadiliano, haki na amani.

Biashara haramu ya silaha ni kikwazo kikubwa katika mchakato wa ujenzi na udumishaji wa Injili ya amani na usalama duniani na hapa kinachopewa kipaumbele cha pekee ni fedha ambayo kwa hakika inanuka damu ya watu wasiokuwa na hatia. Changamoto na dhamana ya Jumuiya ya Kimataifa ni kudhibiti biashara ya silaha duniani. Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kuhimiza mchakato wa ujenzi wa umoja na mshikamano wa kimataifa, ili kuzijengea uwezo nchi changa zaidi duniani katika mchakato wa kukuza na kudumisha uchumi wake.

Kufungwa kwa mipaka ya nchi ni kuwakosea haki wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi, usalama, ustawi na maisha bora zaidi. Hawa ni watu wanaokimbia vita, dhuluma, nyanyaso na mipasuko ya kidini. Hapa kuna haja ya kuamua na kutenda kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima, ustawi na maendeleo ya wengi, kwa kutambua kwamba, wote wanaunda familia kubwa ya watu wa Mungu. Watu wakumbuke kwamba, maisha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inapaswa kukuzwa na kudumishwa. Amani na usalama vinafumbatwa katika fadhila ya unyenyekevu dhidi ya kiburi, kwani vita, misigano pamoja na mipasuko ya kijamii ni matokeo ya kiburi cha binadamu anayetaka kujitutumua na kujionesha kuwa ana nguvu kuliko wengine wote. Bila unyenyekevu hakuna amani na bila amani hakuna umoja wala mshikamano wa kitaifa.

Kardinali Parolin, amepata nafasi pia ya kukutana na kuzungumza na Jumuiya ya Seminari kuu ya Taalimungu, nchini Madagascar. Hii ni kati ya Seminari tano ambazo kwa sasa zina majandokasisi 128 wanaojiandaa kwa ajili ya maisha na utume wa Kipadre. Amekutana na kuzungumza na Askofu Gilbert Aubry, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki La Rèunion ambaye amemwelezea Kardinali Parolin kwa ufupi hali hali ya maisha na utume wa Kanisa Visiwani humo. Ametembelea Kituo cha Akamasoa huko Andralanitra kinachowahudumia watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi zaidi. Familia ya Mungu nchini Madagascar imetoa ombi maalum kwa Baba Mtakatifu Francisko kutembelea Madagascar, ili kuwaimarisha ndugu zake katika imani, upendo na matumaini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.