2017-02-02 11:09:00

Mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa amani duniani!


Chuo Kikuu cha Kikatoliki kinapaswa kuwa ni mahali ambapo panasaidia kukuza na kudumisha mchakato wa mahusiano na mafungamano ya kijamii; mahali pa kunoa akili za vijana wa kizazi kipya ili kuwapatia ujuzi, maarifa na stadi za maisha; ili hatimaye, kuweza kufikia ukomavu wa mtu mzima: kiroho na kimwili sanjari na kujenga madaraja ya watu kukutana kwa njia ya madiliano katika ukweli na uwazi. Chuo kikuu ni mahali pa kuwafunda vijana wa kizazi kipya kanuni maadili na utu wema; umuhimu wa kufanya kazi kwa bidi kama utimilifu wa utu na heshima ya binadamu, tayari kuhiriki katika ujenzi wa jamii inayosimikwa katika misingi ya haki, amani na maridhiano.

Ikumbukwe kwamba, fadhila ya amani inawashirikisha na kuwafungamanisha binadamu wote kwani hiki ni kikolezo cha mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu! Lakini, amani ya kweli inafumbatwa katika: ukweli,haki, upendo na uhuru. Papa Benedikto XV katika Waraka wake wa Kitume “Pacem Dei Munus” anasema, amani ni sehemu muhimu sana ya Mafundisho Jamii ya Kanisa na Diplomasia ya Kimataifa. Haya yamesemwa na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican, Alhamisi tarehe 2 Februari 2017 wakati alipokuwa anatoa mhadhara kwenye Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Sophia, kilichoko Tokyo, Japan, juu ya “umuhimu wa ujenzi wa utamaduni wa amani” wakati wa ziara yake ya kikazi nchini Japan kuanzia tarehe 27 Januari hadi 3 Februari 2017. Baba Mtakatifu Francisko anasema, utamaduni wa amani duniani unahatarishwa na ubinafsi, uchu wa mali na madaraka; umaskini na athari za mabadiliko ya tabianchi. Amani ya kweli inajengwa katika msingi wa maendeleo endelevu ya binadamu: kiroho na kimwili; kanuni maadili na utu wema; utawala wa sheria na haki msingi za binadamu!

Vita, kinzani na mipasuko ya kijamii ni sehemu ya hali halisi ya maisha ya binadamu yanayopswa kufanyiwa kazi kwa kujikita katika kanuni maadili, sheria za kimataifa sanjari na ujenzi wa siasa ya amani duniani inayofumbata majadiliano katika ukweli na uwazi. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuwekeza katika mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa amani duniani; upendo na mshikamano wa dhati; majadiliano pamoja na kusimama kidete kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu, uhuru pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Jumuiya ya Kimataifa iwezeke katika uchumi unaojali na kuzingatia mahitaji msingi ya binadamu, utu na heshima yake.

Vita itaendelea kuibuka sehemu mbali mbali za dunia, ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa haitawajibika barabara kudhibiti biashara haramu ya silaha duniani inayoendelea kupandikiza mbegu ya kifo kwa watu wasiokuwa na hatia! Badala ya kuwekeza katika biashara ya silaha duniani, rasilimali fedha hii ielekezwe zaidi katika sekta ya elimu, afya, ustawi na maendeleo ya wengi, tayari kupambana na umaskini wa hali na kipato! Jambo la msingi ni kujenga mshikamano kati ya mataifa kwa kuongozwa na kanuni auni, mchakato unaoweza kufanikisha hata utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Millenia ifikapo mwaka 2030 kwa ajili ya mafao, ustawi na maendeleo ya familia ya binadamu!

Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican anahitimisha mhadhara wake kwa kusema, lengo ni kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo kwa kuwa na dira ya kinabii inayowakusanya binadamu wote kutoka katika: tamaduni, imani na matabaka mbali mbali ya kijamii tayari kushuhudia huduma katika wema, majadiliano na amani duniani. Mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa amani duniani unafumbatwa katika mafungamano na mahusiano ya kijamii; kwa kujizatiti katika misingi ya haki; umoja, mshikamano na udugu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.