2017-02-02 14:51:00

Mt.John Bosco bado ni msaada kwa matatizo ya vijana na masikini


Ujumbe wa Mtakatifu John Bosco kwa wakati huu  bado unaendelea kuwa msaada kwa vijana katika matatizo au kwenye umasikini. Ni wito wa utume katika kufundisha thamani ya familia kwa ngazi ya kimataifa. Familia ya wasalesiani daima iweza kuendelea katika kufanya mapokezi kwa njia nyepesi , ya upendo wa moja kwa moja kwa familia.Ni  maneno ya Mkurugenzi wa kimisionari wa wa Shirika la Don Bosco, Giampietro Pettenon wakati wa tukio la kuadhimisha siku ya Mtakatifu mwanzilishi wa shirika la wasalesiani ajulikanaye ulimwenguni kote na hasa kutokana na mashule mengi na vituo vya vijana,ni sikukuu inayoandishimwa kila mwaka ifikapo tarehe 31 Januari.Mkurugenzi Pettenon anasema utume huo ndiyo wa kuondoka kwenda katika pembezoni mwa dunia, akikumbuka wamisionari wa kwanza walio kwenda Argentina.


 Na  Makamu wa Rais watu kujitolea  kimataifa kwaajili ya maendeleo endelevu Padre Guido Errico anasema mafundisho ya John Bosco kwa mantiki ya Afrika,vijana wengi wanao utajiri mkubwa utokanayo na furaha ndani ya familia zao  ambayo pia  ndiyo asili ya  kila aina ya matendo ya wasalesiani mahali popote wanapokuwa kwa kuwajibika kwa nguvu zao zote, ili kuweza kukuza matumaini na ubora wa maendeleo endelevu mahali popote wanapotumwa.
Hali kadhalika naye Paola Schinelli anaye jitolea katika ngazi ya kimataifa wa Shirika la Wasalesiani ambaye anafuatilia baadhi ya miradi mbalimbali iliyo anzishwa katika nchi tofauti barani Afrika ya Mashariki kwa mchango wa ushirikiano katika nchi ya Italia , anaonesha ukweli wa thamani na karama ya wasalesiani wa Mtakatifu John Bosco  katika kuendesha mahitaji na mshikamano wa maendeleo.


John Bosco  alizaliwa na Francesco Bosco na Margherita Occhiena tarehe 16 Agosti 1815 karibu na Castelnuovo d'Asti, leo hii inaitwa Castelnuovo Don Bosco. Baba yake alifariki mwaka 1917 akimuachia mke wake na watoto watatu. Ilikuwa miaka migumu kwa maradhi na njaa, lakini mama yake alijitahidi kuwatunza na kuwalea vizuri.Alipokuwa na miaka 9, John alipata ndoto ya kinabii iliyomtabiria utume wake kwa vijana na baadaye Mungu alizidi kumjalia karama nyingi za pekee.
Kufuatana na ndoto hiyo, John aliamua kuwa padri, ingawa hakuweza kusoma hata shule ya msingi, kwa sababu ilikuwa mbali. Lakini taratibu mama alimfanyia mpango dhidi ya upinzani wa kaka yake. Wakati huohuo alianza utume wake akitumia vipawa vyake vyaajabu. Tarehe 26 Machi 1826, siku ya Pasaka, alikubaliwa kupokea ekaristi ya kwanza kabla ya wakati.Kwa ushauri la Yosefu Cafasso tarehe 30 Oktoba 1835 aliingia seminari ya Chieri. Tarehe 3 Novemba 1837 alianza masomo ya teolojia, na tarehe 29 Machi 1841 akapewa daraja takatifu ya ushemasi,ikifuatiwa tarehe 5 Juni 1841 upadri huko Torino.

Badala ya kuitikia mialiko ya kufanya utume wenye malipo mazuri, mnamo Novemba 1841 alijiunga na Bweni la Torino, ambapo padri Luigi Guala, akisaidiwa na Cafasso, alikuwa anakamilisha malezi ya mapadri vijana 45 waweze kukabili ulimwengu wa wakati huo .Huko Torino kulikuwa na watoto 7184 chini ya umri wa miaka 10 waliofanya kazi viwandani. John Bosco aliwatafuta ili kuwasaidia kijamii na kidini. Pamoja na Cafasso alitembelea magereza akashtuka kuona hali ya wafungwa vijana, na kwa wema wake aliwavuta kumuahidia wamfuate mara baada ya kutoka.
Tarehe 8 Desemba 1841 Bartolomeo Garelli alikuwa wa kwanza kujiunga na kundi lake (Oratorio). Muda mfupi baadaye vijana walikuwa wengi hivi hata akahitaji msaada wa mapadri watatu na vijana wakubwa kadhaa.Hatimaye tarehe 12 Aprili 1846 alipata nafasi kwa vijana wake ambacho kilikuwa kibanda na kiwanja huko Valdocco.Yeye alijitahidi hasa kuwaelimisha watoto na vijana wa kiume wakati wa nyakati zake. Mbinu zake za malezi ziliangalia sana akili, dini, hisani. Hakutaka kurekebisha vijana kwa ukali, bali kuwakinga dhidi ya maovu kwa wema. Upendo wake wa ajabu kwa vijana ndio siri ya mafanikio yake ya ajabu katika malezi, na ambayo ameacha rithi mkubwa kwa wafuasi wake kuendeleza utume wake huo popote duniani.


Mwaka 1854 alianzisha shirika la mapadri kwa utume wa vijana (kifupisho chake ni SDB) na miaka 10 baadaye alianza ujenzi mahali patakatifu pa Bikira Maria Msaada wa Wakristo (ndivyo alivyopendelea kumuita mama wa Yesu). Mwaka 1872, pamoja na Maria Domenica Mazzarello, alianzisha shirika la Mabinti wa Bikira Maria Msaidizi, ili walee wasichana kwa roho ileile. Mwaka 1875 alianza kutuma Wasalesiani wa kwanza huko Argentina, na wakati huohuo alianzisha kundi la watawa wasaidizi alio waona kama «Wasalesiani wa nje».John Bosco alifariki tarehe 31 Januari1888 na Papa Pius XI alimtangaza mwenye heri tarehe 2 Juni 1929 na mtakatifu tarehe 1 Aprili 1934.Tangu wakati huo  Sikukuu yake ikawa kila tarehe 31 Januari ya kila mwaka.

 

Sr Angela Rwezaula

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.