2017-02-01 15:11:00

Waamini wasindikizeni mapadre na watawa kwa sala na sadaka zenu!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Siku ya Jumatano, tarehe 1 Februari 2017 amewakumbusha waamini kwamba, tarehe 2 Februari, 2017 Kanisa linaadhimisha Siku kuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni sanjari na Siku ya Watawa Duniani. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwasindikiza Mapadre na Watawa katika maisha na utume wao kwa njia ya sala na sadaka zao. Hawa ni watu ambao maisha yao yote wameyasadaka kwa ajili ya Mungu, Kanisa na jirani. Kumbe, waamini wazidi kuwaombea Mapadre na Watawa, ili kweli huduma ya karama zao za kitawa iweze kuzaa mambo mema kwa waamini pamoja na kusaidia mchakato wa Uinjilishaji unaotekelezwa na Mama Kanisa sehemu mbali mbali za dunia.

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwatambua wajumbe wa Harakati za Kikatoliki za Utunzaji Bora wa Mazingira. Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza kwa kazi kubwa wanayoitekeleza katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Anawataka kuendelea kurusha nyavu zao kwa ujasiri ili hatimaye, Makanisa mahalia yaweze kusikiliza na kujibu kilio cha maskini na utunzaji bora wa mazingira. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini kuendelea kujikita katika umwilishaji wa matendo ya huruma: kiroho na kimwili kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Amewataka wagonjwa na wanandoa wapya kuwasindikiza watawa kwa sala katika maisha na utume wao, ili hawa walioitwa na kufunga nadhiri waweze kuwa ni mashuhuda wenye mvuto na mashiko duniani, kwa kung’arisha upendo wa Kristo na neema ya Injili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili.








All the contents on this site are copyrighted ©.