2017-01-31 10:05:00

Vitendo vya kigaidi ni uhalifu dhidi ya uhai, utu na heshima ya watu


Baba Mtakatifu Francisko amesikitishwa sana na shambulizi la kigaidi lililotokea, Jumapili tarehe 29 Januari 2017 kwenye Kituo cha Utamaduni wa Kiislam Jijini Quebec, nchini Canada na kusababisha watu 6 kupoteza maisha na wengine 8 kupata majeraha makubwa. Baba Mtakatifu, Jumatatu, tarehe 30 Januari 2017 amekutana na kuzungumza na Kardinali Gèrald Cyprien LaCroix na kumhakikishia uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala. Anawaalika Wakristo na Waislam kuendelea kushikamana kwa dhati katika kipindi hiki kigumu cha mpito na majaribu makubwa! Kardinali Gèrald Cyprien LaCroix aliyekuwa mjini Roma kwa shughuli maalum amerejea nchini Canada kwenda kufuatilia tukio hiki kwa karibu zaidi.

Baba Mtakatifu Francisko katika salam za rambi rambi zilizoandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Kardinali Gèrald Cyprien LaCroix, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Quebec, Canada, anasema, anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa watu wote walioguswa na kutikiswa na shambulizi hili la kigaidi. Anamwomba Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na upendo, aweze kuwafariji wote. Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii kulaani vitendo vyote vya kigaidi vinavyodhalilisha utu na heshima ya binadamu. Anamwomba Mwenyezi Mungu aweze kuwakirimia waamini zawadi ya amani na kuheshimiana.

Wakati huo huo, Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini katika taarifa yake linasema, limesikitishwa sana ni shambulizi hili la kigaidi dhidi ya waamini wa dini ya Kiislam waliokuwa wana swali huko Jijini Quebec. Vitendo hivi ni kufuru dhidi ya maisha, utu na heshima ya binadamu. Hawa ni waamini waliokuwa wanaswali. Baraza hili linapenda kutumia fursa hii kulaani vikali vitendo vyote vya kigaidi na linataka kuonesha mshikamano wa dhati na waamini wa dini ya Kiislam nchini Canada, kwa kuwahakikishia sala na dua kwa wahanga wa vitendo hivi vya kigaidi.

Kwa upande wake, Bwana Justin Trudeau, Waziri mkuu wa Canada amelaani vikali shambulizi hili na kusema kwamba, hivi ni vitendo vya kigaidi dhidi ya waamini wa dini ya Kiislam waliokuwa wanaswali Msikitini pamoja na wakimbizi na wahamiaji kupatiwa hifadhi katika Kituo cha Utamaduni wa Kiislam Jijini Quebec. Anasema, tofauti za wananchi wa Canada ni nguvu na jeuri ya wananchi wote wa Canada.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.