2017-01-31 10:41:00

Maaskofu wa DRC wana matumaini na wanasiasa!


Baraza la Maaskofu Katoliki Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo linasema lina matumaini makubwa katika utekelezaji wa mkataba wa amani uliotiwa sahihi tarehe 31 Desemba 2016 kati ya Serikali na Vyama vya upinzani ili kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa chini ya Rais Joseph Kabila atakayesimamia kipindi cha mpito hadi uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka 2017. Katika kipindi hiki cha mpito Waziri mkuu atateuliwa miongoni mwa Vyama vya Upinzani na kwamba, Rais Kabila hataweza kuwania tena madaraka.

Maaskofu wanasema, huu ni wakati wa kutekeleza kwa vitendo yale mambo msingi yaliyoamriwa ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya wananchi wa DRC. Hayo yamebainishwa na Askofu mkuu Fridolin Ambongo Besungu, Makamu wa Rais Baraza la Maaskofu Katoliki DRC ambaye pamoja na ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki DRC unatembelea Barani Ulaya. Baraza la Maaskofu Katoliki DRC linaendelea kutoa nafasi kwa wanasiasa nchini DRC kuamua kwa dhati kabisa mustakabali, ustawi na maendeleo ya wananchi wa DRC kwa kujikita katika demokrasia, ukweli na uwazi. Bado hadi sasa kuna vuta nikuvute miongoni mwa wanasiasa, lakini Maaskofu wanawataka wanasiasa wote kufanya maamuzi magumu kwa ajili ya mafao ya wengi!

Na Padre Richard A. Mjigwa C. PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.