2017-01-30 14:49:00

Watawa mnapaswa kuwa ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu


Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican kuanzia tarehe 27 Januari hadi tarehe 3 Februari 2017 anafanya ziara ya kikazi nchini Japan. Jumamosi tarehe 28 Januari 2017 ameadhimisha Siku ya Watawa nchini Japan, kwa kuwakumbuka Wamissionari wa kwanza waliojisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu nchini Japan, kiasi cha kujenga madaraja yanayowakutanisha watu na tamaduni mbali mbali ili kushirikishana furaha ya imani inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa, kiini cha imani na miito ya kitawa ndani ya Kanisa.

Kristo Yesu amekuja ulimwenguni ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, dhamana inayoendelezwa na Mama Kanisa. Yesu Kristo ni Kuhani mkuu mwenye rehema, mwaminifu katika mambo ya Mungu na mpatanishi kati ya Mungu na binadamu, changamoto kwa watawa kuwa kweli ni mwanga, mashuhuda na vyombo vya upendo na huruma ya Mungu kwa watu wa mataifa, kwani wameitwa na ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Kwa njia ya karama na mapaji ya Roho Mtakatifu, watawa wanashiriki kikamilifu: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo katika maisha na utume wao.

Askofu Mkuu Paul Richard Gallagher anawakumbusha watawa kwamba, wito wao ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, walioupata kwa kukutana na kushibana na Kristo Yesu, kiasi hata cha kuamua kumfuasa katika maisha yao yote, huku wakijitahidi kila siku kufanana na Kristo Yesu, Kuhani mkuu. Ili kupalilia na kukuza miito mitakatifu ndani ya Kanisa kuna haja kwa watawa kujenga Jumuiya za imani inayomwilishwa katika utume wa Kanisa wenye mvuto na mashiko, kiasi hata cha kuweza kuwamegea vijana wa kizazi kipya furaha ya Injili inayobubujika kutoka katika undani wa maisha ya waamini.

Watawa wajenge na kudumisha umoja wa imani, kwa njia ya ushuhuda wa uwepo endelevu wa Kristo Yesu katika maisha yao. Wawe wasikivu kwa Roho Mtakatifu, daima wakijitahidi kusoma alama za nyakati, ili kweli waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda huruma, msamaha na upatanisho kati ya watu! Watawa anasema, Askofu mkuu Paul Richard Gallagher wanapaswa kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake, kila mmoja kadiri ya karama na mapaji aliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu, kama sehemu ya mchakato wa mwendelezo wa kazi ya Ukombozi! Watawa wakijiaminisha kwa Kristo watakuwa kweli  ni mashuhuda na vyombo vya furaha ya Injili na wajenzi makini wa Ufalme wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.