2017-01-28 15:38:00

Vijana wa Kiluteri Duniani kukutana nchini Namibia Mei, 2017


Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani, litafanya mkutano wake mkuu wa kumi na mbili  huko Windhoek, Namibia kuanzia tarehe 10 – 16 Mei 2017. Mkutano huu utatanguliwa na mkutano wa Vijana wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri kutoka sehemu mbali mbali za dunia watakaoanza kikao chao tarehe 3 – 9 Mei, 2017, kama sehemu ya mkesha! Huu ni mkutano ambao utafumbatwa katika tunu za kiutu “Ubuntu” unaofumbata kwa namna ya pekee: huruma, upole, upendo na mshikamano kama anavyofafanua Mchungaji Helvi Muremi, mjumbe wa Kamati ya Maandalizi ya Mkutano mkuu wa XII wa Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani.

Taarifa inabaisha kwamba, zaidi ya vijana 110 kutoka katika nchi 70 wanatarajiwa kushiriki katika mkutano huu, sanjari na kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani. Hii ni fursa kwa vijana kuweza kushirikishana: uzoefu, mang’amuzi, matatizo, furaha na changamoto za maisha ya ujana kutoka sehemu mbali mbali za dunia pamoja na kujionea wenyewe changamoto ya vijana wa Namibia katika maisha yao ya kila siku!

Mchungaji Wynand Lukas, Rais wa Kamati ya maandalizi ya mkutano mkuu wa Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani anasema, vijana wa kizazi kipya wanataka maboresho makubwa katika masuala ya uchumi na kijamii; wanataka kuona mfumo wa elimu bora na sawa utakaowajengea uwezo wa kupambana na mazingira, ili kuyageuza kuwa ni mahali bora zaidi pa kuishi. Vijana wanatamani kupata fursa za ajira ili kutekeleza ndoto za maisha yao ya ujana, kwani waswahili wanasema, ujana mali, fainali uzeeni!

Lakini, vijana wanakumbushwa kwamba, ujana wakati mwingine ni sawa na kichwa cha mwendawazimu, kwani wasipokuwa macho na makini, watajikuta wanatumbukia au kutumbukizwa katika ulevi wa kupindukia, ukahaba pamoja na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo kama vile: matumizi haramu ya dawa za kulevya; mimba za utotoni, maambukizi ya Ukimwi; biashara haramu ya binadamu na viungo vyake bila kusahau athari za mabadiliko ya tabianchi. Hizi zote ni changamoto zinazopaswa kusimamiwa kidete ili kuwajengea vijana msimamo thabiti katika maisha.

Mkutano wa Vijana wa Kiluteri Duniani, utakuwa ni sehemu ya maandalizi ya mkutano mkuu wa Shirikisho la Makanisa ya Kiluteri Duniani sanjari na maadhimisho ya Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani. Kumbe, viongozi wakuu wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri wanapenda kuchukua nafasi hii kuwahamasisha vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia kujitokeza kikamilifu ili kujifunza, kushirikishana na kukumbushana kwamba, wamekombolewa kwa njia ya neema ya Mungu. Mkutano huu unatanguliwa na mikutano ya kikanda huko mjini Hoor, nchini Sweden kuanzia tarehe 31Januari hadi 2 Februari 2017, kwa ajili ya Kanda ya Bara la Ulaya;  Johannesburg, Afrika ya Kusini kuanzia tarehe 5 - 11Februari 2017 kwa ajili ya Kanda ya Afrika. Kutakuwa pia na mkutano wa Wanawake wa Kiluteri Duniani kuanzia tarehe 4- 9 Mei 2017 huko Windhoek, Namibia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.