2017-01-28 12:18:00

Ujumbe wa Siku ya Kupambana na Ugonjwa wa Ukoma Duniani 2017


Jumuiya ya Kimataifa tarehe 29 Januari 2017 inaadhimisha Siku ya Kupambana na Ugonjwa wa Ukoma Duniani kwa kuongoza na kauli mbiu “Utokomezaji wa ugonjwa wa Ukoma na kuwaingiza tena waathirika katika jamii ni changamoto endelevu”. Takwimu zinaonesha kwamba, kunako mwaka 1985 watu zaidi ya milioni tano walikuwa wameathirika kutokana na ugonjwa wa Ukoma duniani na kwamba, kila mwaka duniani kuna wagonjwa wapya laki mbili, changamoto ambayo inahitaji kuvaliwa njuga na wadau mbali mbali!

Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu katika ujumbe kwa maadhimisho ya Siku ya 64 ya Mapambano ya Ugonjwa wa Ukoma Duniani kwa Mwaka 2017 anasema, maambukizi mapya ya ugonjwa wa Ukoma ni hatari kwa utu na heshima ya binadamu, kwani wengi wao wanabaguliwa, wanatengwa na kunyanyapaliwa na jamii. Wadau mbali mbali kwa kushirikiana na Mfuko wa Afya wa Sasakawa kutoka Japan, Jeshi la Malta, Mfuko wa Raoul Follereau pamoja na Mfuko wa Msamaria mwema, wanaendelea kuhimiza umuhimu wa viongozi wa kidini kusaidia kuelimisha umma dhidi ya tatizo la kuwabagua na kuwanyanyapalia wagonjwa wa Ukoma duniani.

Changamoto hii pia inavaliwa njuga na Shirika la Afya Duniani, WHO, linalowataka wafanyakazi katika sekta ya afya kuhakikisha kwamba wagonjwa waliopona Ukoma wanahudumia na kusaidiwa kisaikolojia pamoja na kuondokana na sheria zinazowabagua wagonjwa wa Ukoma kutoka katika medani mbali mbali za maisha ya kijamii. Serikali zinapaswa kupanga sera na mikakati itakayowashirikisha waliokuwa wagonjwa wa Ukoma katika maisha ya kijamii sanjari na kuboresha vifaa vya tiba na uchunguzi wa ugonjwa wa Ukoma, ili kuweza kuudhibiti ukiwa bado katika hatua za mwanzo kabisa pamoja na kuweka mikakati ili wagonjwa waliobainika wanapata tiba kamili bila kusitisha kwani hii ni kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao na jamii inayowazunguka, ili hatimaye, kuweza kuingizwa katika jamii yao ili kuendelea na maisha kama kawaida.

Kardinali Turkson anasema, juhudi hizi zinapaswa kuungwa mkono na wadau mbali mbali na kwamba, kuna mafanikio ambayo yamekwisha kupatikana katika nchi kama vile: India, Brazil na Ghana ambako familia zilizokuwa zimeathirika zilielimishwa vyema, kiasi cha kuunda mazingira ya kuwapokea na kuwaingiza tena wagonjwa wa Ukoma waliopona, kiasi cha kujenga udugu wa kweli.  Yesu katika maisha na utume wake, aliwaonea huruma wakoma, akawagusa, akawaponya na kuwarejesha tena katika maisha ya kawaida katika jamii zao.

Hii ni changamoto pevu kwa jamii nyingi katka ulimwengu mamboleo, kuweza kuwaingiza watu wenye alama za ugonjwa wa Ukoma katika maisha ya kawaida. Hii inatokana na ukweli kwamba, ugonjwa wa Ukoma ni kati ya magonjwa yanayoogopwa sana duniani. Hii inatokana na ukosefu wa taarifa makini juu ya ugonjwa huu; ubaguzi unaofanywa kwa wale waliopona lakini wakaendelea kubakia na makovu; kiasi cha kujisikia kutengwa na hivyo kukosewa utu na heshima yao kama binadamu. Kumbe, anasema Kardinali Peter Turkson, kuna haja ya kusimama kidete pamoja na waathirika wa ugonjwa wa Ukoma kupambana ili hatimaye, waweze kukaribishwa, kuoneshwa haki na mshikamano wa kidugu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.