2017-01-28 10:33:00

Kanisa nchini Italia linataka kuwa karibu na watu kwa ajili ya watu!


Baraza la Maaskofu Katoliki Italia limehitimisha mkutano wake uliofanyika hivi karibuni na kusema kwamba, Kanisa nchini Italia litaendelea kushikamana na familia ya Mungu nchini humu ambayo kweli imejaribiwa na kutikiswa kutokana na majanga asilia ambayo yanaendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Hali hii inaendelea kugumishwa pia kutokana na athari za myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa.

Katika shida na mahangaiko ya watu, Kanisa linataka kuonesha mshikamano wake wa upendo na ukaribu kwa wote walioathirika anasema, Askofu Nunzio Galantino. Kwa namna ya pekee kabisa, Kanisa linataka kuwa ni mhimili mkuu wa familia pamoja na kuwa ni sauti ya watoto wakimbizi na wahamiaji wanaojikuta wako pweke bila msaada wa wazazi na walezi wao; hali inayohatarisha usalama, ustawi na maendeleo ya watoto hawa kwa sasa na kwa siku za usoni. Baraza la Maaskofu Katoliki Italia limeonesha wasi wasi wake kutokana na muswada wa sheria unaotaka kuhalalisha utamaduni wa kifo kwa kukumbatia kmchakato wa kifo laini.

Maaskofu wa Italia kwa namna ya pekee, wameguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya watu waliotikiswa kwa majanga asilia na kwa sasa wanaishi katika mazingira magumu na hatarishi. Ni watu ambao umaskini uko mbele ya uso wao kutokana na kupoteza makazi na mitaji ya miradi yao iliyokuwa inawapatia kipato cha maisha. Maaskofu wanawapongeza wananchi waliokumbwa na majanga asilia, jinsi wanavyokabiliana na changamoto hii kwa ujasiri, ari na moyo mkuu pasi na kukata tamaa.

Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki nchini Italia, Caritas Italia, yataendelea kutoa huduma kwa waathirika wa majanga asilia nchini Italia, kielelezo cha uwepo wa karibu wa Kanisa kwa waathirika hawa. Hadi sasa kiasi cha Euro milioni 22 zimekwisha kusanywa kwa ajili ya  kutoa msaada kwa waathirika wa majanga asili anchini Italia. Fedha hii itatumika kwa ajili ya ujenzi wa miundo mbinu ya huduma, mahitaji msingi pamoja na kugharimia miradi ya maendeleo na ustawi wa jamii. Lengo pia ni kushirikiana na serikali katika kuendeleza mchakato wa kukarabati Makanisa yaliyoharibiwa vibaya na matetemeko ya ardhi yaliyojitokeza hivi karibuni nchini Italia.

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linapenda kuwa ni sauti ya familia zinazoteseka kutokana na majanga asilia pamoja athari za myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa, ili kweli wanasiasa na watunga sera waweze kujizatiti zaidi katika kuziwezesha kiuchumi familia hizi, ili hatimaye, ziweze kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara. Kumbe, hapa jambo la msingi ni kuibua mbinu mkakati utakaowawezesha watu kupata ajira.

Maaskofu pia wamejadili kwa kina na mapana maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana kwa mwaka 2018 itakayoongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito”. Hii ni tema itakayopembuliwa na Maaskofu wa Italia katika mkutano wake utakaofanyika kuanzia tarehe 22- 25 Mei 2017. Sera na mikakati  makini ya shughuli za kichungaji kwa vijana, elimu na majiundo makini ni kati ya mambo yatakayochambuliwa kama “karanga” wakati wa mkutano huo. Maaskofu wanasema, majiundo ya awali na endelevu kwa wakleri yataendelea kupewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Kanisa. Lengo ni kukazia maisha ya kiroho, ari na moyo wa kitume na kimissionari. Itakuwa ni nafasi pia ya kuangalia sheria na kanuni za kuendesha Mahakama za Kanisa nchini Italia mintarafu kesi za ndoa na familia. Mada hii itaendelea kuchambuliwa pia na Maaskofu kwenye mikutano yao ijayo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.