2017-01-27 11:12:00

Wakristo wanapaswa kushikamana ili kukabiliana na changamoto za dunia


Majadiliano ya kiekumene yanafumbatwa katika imani na mapendo kwa kumwangalia jirani kwa njia ya miwani ya imani, ili kuondokana na tabia ya kudhaniana vibaya na malumbano yasiyokuwa na tija wala mashiko kwa familia ya Mungu. Hii ni sehemu ya ujumbe ulioandikwa na Kardinali Peter Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya binadamu kwa wajumbe wa Baraza la Jukwaa la Wakristo kwa ajili ya huduma za kichungaji kwa wanasarakasi na michezo ya watoto.

Viongozi wa Jukwaa hili walikuwa kwenye mkutano wao wa mwaka uliofanyika kuanzia tarehe 22 - 24 Januari 2017 kama sehemu pia ya maadhimisho ya Juma la Kuombea Umoja wa Kanisa, huko kwenye Ufalme wa Monaco. Mkutano huu umefanyika pia wakati wa Tamasha la Sarakasi Kimataifa huko Monte Carlo. Kardinali Peter Turkson, anakaza kusema, majadiliano ya kiekumene yanapania kuwasaidia wakristo kushikamana ili kuweza kukabiliana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo hasa kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu; usawa, utu na heshima ya binadamu, kwa kutambua kwamba, wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Mkutano huu umeongozwa na kauli mbiu “Tuko pamoja kwa ajili ya majadiliano”. Lengo kuu ni kuendelea kuimarisha umoja, mshikamano na majadiliano ya kidugu; yanayofumbatwa katika ukweli na uwazi; heshima, uvumilivu pamoja na ukarimu. Haya ni mambo msingi yanayopewa kipaumbele cha pekee na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kichungaji “Laudato si”  yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”.

Baba Mtakatifu anawahamasisha wadau mbali mbali kushikamana ili kutafuta suluhu ya changamoto katika ulimwengu mamboleo. Majadiliano ya kweli ni msingi wa mahusiano na mafungamano kati ya mtu na mtu yanayosaidia anasema Baba Mtakatifu kujenga utamaduni wa watu kukutana. Hii ni sehemu ya mchakato unaopania kujenga na kudumisha majadiliano, uhusiano na umoja na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani. Ili kufikia hatua hii, binadamu ana haja ya kukua, kukomaa na kujitakatifuza. Kardinali Peter Turkson anakamilisha ujumbe wake kwa kusema, mchakato wa watu kukutana unasaidia pia mwingiliano wa watu, kiasi hata cha kubadilishana karama na zawadi kutoka Mwenyezi Mungu, kuendelea kudumisha udugu katika mwanga wa Roho Mtakatifu, ili kuwaelekeza waamini katika ukweli, upatanisho na uponyaji wa mahusiano yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.