2017-01-26 08:18:00

Maadhimisho ya Siku ya XXI ya Watawa Duniani 2017


Katika maadhimisho ya Siku kuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni, hapo tarehe 2 Februari 2017 sanjari na maadhimisho ya Siku ya XXI ya Watawa Duniani iliyoanzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kuanzia saa 11: 30 za jioni kwa saa za Ulaya. Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume linasema, maadhimisho ya Mwaka huu yanapata umuhimu wake wake kama fursa makini ya kushukuru na kusali kwa ajili ya kuombea zawadi ya miito mintarafu maandalizi ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu vijana itakayoadhimishwa kunako mwaka 2018. Itakumbwa kwamba, Sinodi hii inaongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya miito!

Hapa kwa namna ya pekee kabisa, vijana wanahamasishwa na Mama Kanisa kushiriki katika maandalizi haya na hatimaye, kuweza kufanya maamuzi magumu katika maisha yao kwa kumfuasa Kristo kwa ukaribu zaidi katika maisha ya Kipadre, Kitawa au ndoa, kwa kujitosa bila ya kujibakiza. Kwa njia hii, anasema Baba Mtakatifu Francisko sadaka na majitoleo haya yanakuwa kama chemchemi ya maji iliyofichika chini ya ardhi kwa muda mrefu na inasubiri kuibuka na kuanza kuwapatia watu maji safi na baridi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.