2017-01-25 14:46:00

Dr. Buzzonetti apumzishwa kwenye usingizi wa amani!


Dr. Renato Buzzonetti katika maisha yake kama mwamini alijitahidi kumwilisha imani yake kwa Kristo na Kanisa lake, kiasi kwamba, ikawa ni sehemu ya ushuhuda wa kazi yake kama daktari wa binadamu. Vatican ina deni kubwa mbele ya Dr. Renato Buzzonetti aliyewahudumia: Mwenyeheri Paulo VI, Papa Yohane Paulo I, Mtakatifu Yohane Paulo II pamoja na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI, hadi alipong’atuka kutoka katika huduma kunako mwaka 2009.  Dr. Buzzonetti katika Ukristo wake alionesha na kushuhudia umuhimu wa kazi kama utumilifu wa utu na heshima ya binadamu; alionja magumu na changamoto za maisha na hasa zaidi za wagonjwa wake; alijikita katika upendo kwa Injili ya uhai; akapambana kikamilifu na magonjwa yaliyokuwa yanawaandama binadamu; alikuwa na mipango pamoja na matumaini katika maisha! Lakini, Injili ya Kristo pia inafumbatwa katika adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu; Uaminifu, Umoja na Upendo wa kidugu!

Kumbe, maamuzi ya mwamini yanapaswa kuzingatia kanuni na taratibu za Kiinjili ili kuweza kujipatia maisha ya uzima wa milele. Jambo la muhimu katika maisha ya Kikristo ni utii kwa Kristo na Kanisa lake na hamu ya kupata maisha ya uzima wa milele. Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Askofu mkuu Georg Ganswein, Msimamizi mkuu wa nyumba ya Kipapa wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumsindikiza Dr. Renato Buzzonetti katika usingizi wa milele baada ya kukunja kilago cha maisha ya hapa duniani. Ibada hii imeadhimishwa tarehe 23 Januari 2017 kwenye Kanisa la Moyo Mtakatifu wa Yesu, Jimbo kuu la Roma na kuhuduhuriwa na umati mkubwa wa familia ya Mungu.

Askofu mkuu Georg Ganswein anakaza kusema, Dr. Buzzonetti alitenda mambo makubwa katika utume wake kama daktari wa binadamu, lakini yote haya ni bure ikilinganishwa na moyo na upendo wake kwa Kristo Yesu na Kanisa lake; sadaka na majitoleo yake kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro; upendo na uaminifu wake uliomwilishwa katika maisha ya kila siku kama mwamini kwa kushiriki sala, Ibada ya Misa Takatifu alimojichotea nguvu ya Neno la Mungu na chakula cha kiroho ili kujenga na kudumisha umoja wa Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa kwa njia ya huduma yake kama daktari.

Maisha na utume wa Kanisa unawaambata wote, maskini na matajiri; wakubwa kwa wadogo, wote hawa wanamkimbilia Mama Kanisa ili kupata Neno, Chakula, Amani na Msamaha wa dhambi. Katika mawazo na mwelekeo kama huu, waamini wanapaswa kujivika fadhila ya unyenyekevu na heshima kwa ndugu na jirani zao katika Kristo Yesu. Kwa namna ya pekee, viongozi wakuu wa Kanisa tangu wakati wa maisha na utume wa Mtakatifu Yohane Paulo II, wasaidizi wa karibu wa Mtakatifu Yohane Paulo II pamoja na wafanyakazi wa Kitengo cha Afya cha Vatican walishiriki kikamilifu, huku wakikumbuka mchango na ushuhuda wa maisha uliotolewa na Dr. Renato Buzzonetti enzi ya uhai wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.