2017-01-24 08:01:00

Ulaya: Bomoeni kuta za uchoyo na ubinafsi ili kuokoa maisha ya watu!


Wakimbizi na wahamiaji ni changamoto pevu inayopaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake kwa kuibua mbinu mkakati utakaosaidia kudhibiti kwa kiasi kikubwa mambo yanayochangia wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani kwa wakati huu. Vita, kinzani, mipasuko ya kidini na kijamii pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi ni kati ya mambo yanayoendelea kuchangia uwepo wa wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani.

Badala ya kujenga kuta zinazojikita katika ubinafsi, kuna haja ya kujenga madaraja ya watu kukutana na kusaidiana kwani hata wakimbizi na wahamiaji ni rasilimali watu na nguvu kazi inayoweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu! Askofu mkuu Vincent Landel wa Jimbo kuu la Rabat, Morocco anapenda kutoa wito na mwaliko kwa familia ya Mungu Barani Ulaya, kufungua malango ya mipaka na nyoyo zao, ili kuwakaribisha na kuwakirimia wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi Barani Ulaya.

Askofu mkuu Landel anasikitika kusema, Bara la Ulaya limegubikwa kwa “blanketi la ubinafsi” linalozifanya baadhi ya nchi kushindwa kuonesha ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotaka kusalimisha maisha yao na badala yake wanatumia fedha nyingi kujenga kuta za utengano. Askofu mkuu Landel ameyasema haya hivi karibuni alipokuwa anazungumza na viongozi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia kuhusiana na hali ya wakimbizi na wahamiaji wanaohudumiwa nchini Morocco, hasa zaidi watoto ambao wanajikuta ni wakimbizi na wahamiaji bila ya kusindikizana na wazazi au walezi wao.

Askofu mkuu Landel anasema, Caritas Morocco inahudumia kambi kubwa tatu zinazotoa huduma ya kuwapokea na kuwakirimia wakimbizi na wahamiaji kutoka Kusini mwa Jangwa la Sahara. Kambi hizi ziko huko: Rabat, Casablanca pamoja na Tangeri. Katika kambi hizi wakimbizi na wahamiaji wanapewa mahitaji msingi ya maisha; wanasindikizwa na kuwahabarisha huduma zinazotolewa kambini humo. Caritas Morocco imeibua mbinu mkakati wa ushirikiano na waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kwa ajili ya kuwahudumia watoto wahamiaji na wakimbizi wanaohitaji msaada zaidi.

Katika mazingira kama haya ya watu waliokata na kujikatia tamaa, kuna vitendo vya uvunjaji wa haki msingi za binadamu; dhuluma na nyanyaso dhidi ya watoto na wanawake; hali inayowageuza baadhi ya watoto na wanawake kuwa kweli ni waathirika wakuu wa utumwa mamboleo wanaotumbukizwa hata wakati mwingine kwenye biashara haramu ya binadamu na viungo vyake; biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya! Lengo kubwa la wakimbizi na wahamiaji wanaopitia nchini Morocco ni kwenda Barani Ulaya mapema iwezekanavyo!

Wanatambua kwamba, mbele yao wanaweza kukabiliana na kifo maji baharini na utupu, lakini wakiangalia mateso waliyokumbana nayo katika nchi zao, wanaamua kupiga moyo konde na kusonga mbele ili kukabiliana na changamoto hii pevu katika maisha yao. Hawa ni watu wanaotafuta hifadhi, usalama na maisha bora kwa familia zao ndiyo maana wanathubutu hata kuhatarisha maisha yao, kwa matumaini kwamba, iko siku wataweza kufanikiwa. Askofu mkuu Vincent Landel anahitimisha kwa kuiomba familia ya Mungu Barani Ulaya kufungua malango ya upendo, ukarimu na huduma kwa wakimbizi na wahamiaji badala ya kujifungia katika kuta na ngome za ubinafsi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.