2017-01-24 08:46:00

Simameni kidete kutetea na kudumisha Injili ya familia!


Familia ni Kanisa dogo la nyumbani ni kitovu cha maendeleo endelevu ya binadamu; shule ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kweli! Hapa ni mahali pa kujifunza tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kijamii, tayari kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ujenzi wa jamii inayojikita katika haki, amani, udugu na upendo. Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani kwa kutambua na kuthamini Injili ya familia katika ustawi na maendeleo ya wengi, wanawataka wanasiasa na watunga sera nchini Ujerumani kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha tunu msingi za maisha ya familia.

Haya ni mambo msingi ambayo yamo kwenye Hati ya Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani kwa ajili ya kulinda, kutetea na kudumisha tunu msingi za familia iliyozinduliwa hivi karibuni huko Dulseldorf na Maaskofu Katoliki Ujerumani ambao pia wameshutumu sera na mikakati ya kisiasa inayokwenda kinyume cha Injili ya familia. Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani linasema, linataka kusimama kidete kulinda, kutetea na kuwahamasisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya familia inayofumbatwa katika Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo!

Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani linawataka wanasiasa kujizatiti zaidi katika sera na mikakati inayopania kudumisha tunu bora za maisha ya kifamilia. Tafiti na upembuzi yakinifu uliofanywa na Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Ujerumani pamoja na taasisi mbali mbali zinazoendeshwa na Kanisa Katoliki nchini Ujerumani unaoesha kwamba, tunu msingi za maisha ya kifamilia ziko hatarini kutokana na sera na mikakati ya kisiasa inayokinzana na Injili ya familia.

Maaskofu wanakumbusha kwamba, ustawi na maendeleo ya Ujerumani yanafumbatwa kwa namna ya pekee katika msingi wa maisha bora ya familia nchini humo! Bila familia, hakuna ustawi, maendeleo na kwamba, matumaini ya Ujerumani kwa siku za usoni, yatafifia na kutoweka kama “nyota ya alfajiri”. Kiwango cha uamskini wa watoto katika familia nyingi nchini Ujerumani kinaendelea kuongezeka siku kwa siku kutoka katika asilimia 1. 6 ya Mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 18. 6 katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita. Hii ni sawa na kila mtoto mmoja kati ya watoto watano kwenye familia anaishi katika hali ya umaskini, hali ambayo ni hatari sana kwa ustawi na maendeleo ya watoto kwa siku za usoni!

Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani linakiri kwamba, kumekuwepo na sera na mikakati ya Serikali kwa ajili ya kuwasaidia watoto wadogo, lakini sera hizi bado hazifui dafu hata kidogo na matokeo yake ni kuongezeka kwa umaskini miongoni mwa watoto wadogo nchini Ujerumani. Hii ni changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga mapema iwezekanvyo wanasema Maaskofu Katoliki wa Ujerumani kabla mambo hayajaharibika zaidi. Anasema, Askofu Franz-Josef Overbeck wa Jimbo Katoliki Essen kwamba, kutokana na kuongezeka kwa kiwango cha umaskini wa familia, hata kiwango cha umaskini miongoni mwa watoto wadogo kimeongezeka maradufu. Hati ya Kulinda na Kutetea Familia nchini Ujerumani, inaitaka Serikali kuongeza vituo vya huduma ya ushauri kwa familia, ili hatimaye, kusaidia ujenzi wa awamu mpya ya maisha ya kifamilia ndani ya jamii. Serikali inapaswa pia kuwekeza zaidi katika huduma kwenye vituo vya kulelea watoto wadogo, kwa kuzingatia muda wa kuanza na kufunga vituo hivi ili kuwasaidia wazazi na walezi kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao katika jamii!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.