2017-01-24 07:38:00

Mambo msingi katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene!


Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la kuhamasisha Umoja wa Wakristo anasema, kumekuwepo na mafanikio makubwa katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene, tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipoyapatia kipaumbele cha pekee na kufanyiwa kazi na viongozi wakuu wa Kanisa waliofuatia. Hawa ni Mwenyeheri Paulo VI, Yohane Paulo II, Benedikto XVI na sasa Baba Mtakatifu Francisko.

Kwa wale waliozoea kusafiri na ndege wanaweza kudhani kwamba, ndege imesimama, lakini inaendelea kusafiri na kwamba, Wakristo wanatumaini kuwa iko siku ndege ya majadiliano ya kiekumene itaweza kutua na Wakristo kushangilia umoja wa Kanisa unaoonekana. Lakini, ikumbukwe kwamba, rubani mkuu wa ndege ya majadiliano ya kiekumene ni Roho Mtakatifu, aliyeanzisha mchakato huu na kwa hakika ataweza kuufikisha bandari salama.

Maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican yaliibua matumaini makubwa miongoni mwa Wakristo na wengi wakatamani kuona umoja kamili wa Kanisa mara moja, lakini hadi sasa imekwisha gota miaka zaidi ya 50. Safari ya majadiliano ya kiekumene anasema Baba Mtakatifu Francisko inafanyika kwa kutembea pamoja, ni ndefu, wakati mwingine inachosha na kuonekana kuwakatisha watu tamaa, lakini Wakristo hawana budi kujifunga kibwebwe kuhakikisha kwamba, wanasonga mbele na safari hii licha ya changamoto na matatizo wanayoweza kukutana nayo njiani kwani kuna mambo mengi yanayowaunganisha, ikilinganishwa na yale yanayowatenganisha kama Wakristo!

Kardinali Kurt Koch anaendelea kufafanua kwamba, upatanisho wa kiukemene hauna budi kwanza kabisa kufumbatwa katika hija inayowahusisha Wakristo na Jumuiya zao. Safari hii inafanyika katika uhalisia wa maisha ya kila siku; kwa kutembea na kuwa pamoja katika mambo msingi yanayoweza kuwaunganisha kama Wakristo yaani katika sala, ushuhuda wa huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Huu ndio mtazamo unaovaliwa njuga na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake. Umoja wa Wakristo si tukio la muujiza, bali ni mchakato wa hija ya pamoja inayoongozwa na Roho Mtakatifu.

Majadiliano ya kiekumene ni dhamana nyeti na pevu, inayowataka Wakristo kujizatiti kweli kweli kwa kujiachilia mikononi mwa Roho Mtakatifu, ili aweze kuwaongoza ili hatimaye, aweze kuwafikisha bandari salama. Ni safari yenye machungu na magumu yake. Kumbe, majadiliano ya kiekumene yanafumbatwa katika ushiriki mkamilifu katika maisha ya jirani, wakati wa raha na uchungu; wakati wa matumaini na wakati wa kukata tamaa kwa kutambua kwamba, wote ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa.

Kwa bahati mbaya, wakati huu, majadiliano ya kiekumene yanashuhudia nyanyaso, dhuluma, mateso na mauaji ya Wakristo sehemu mbali mbali za dunia, lakini hasa zaidi huko Mashariki ya Kati, ambako kumegeuka kuwa ni Ukanda wa mashuhuda wa imani. Huu ni uekumene wa damu kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko. Dhuluma na nyanyaso hizi hazibaguui wala kuchagua huyu ni Mkristo wa Kanisa gani! Wafiadini hawa ni ushuhuda makini wa mchakato wa Uekumene wa damu unaowaunganisha Wakristo badala ya kuwagawa! Katika mauaji, dhuluma na nyanyaso anasema Baba Mtakatifu Francisko hapa kuna changamoto kubwa ya Uekumene wa damu unaowaunganisha hasa zaidi katika kifo. Hii ni changamoto ya kuhakikisha kwamba, Uekumene wa damu unapewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Kanisa, ili kuendelea kuwaunga mkono Wakristo wanaoteseka sehemu mbali mbali za dunia kwa hali na mali!

Kardinali Kurt Koch anasema, majadiliano ya kiekumene yanajikita kwa namna ya pekee katika kulisoma, kulitafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha ya watu kama kielelezo cha imani kwa Kristo na Kanisa lake. Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Duniani linaadhimisha Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani. Haya ni mageuzi yaliyofumbatwa katika kutambua umuhimu wa Neno la Mungu katika maisha ya Wakristo. Neno la Mungu liwawezeshe Wakristo kulitambua Fumbo la huruma na upendo wa Mungu lililofunuliwa kwa njia ya Kristo Yesu ili waweze kuona njia inayowaunganisha tena ili kumwendea Kristo ambaye ni njia, ukweli na uzima.

Kama ilivyokuwa kwa wafuasi wa Emmau, waliweza kugundua na kuonja uwepo wa Kristo Mfufuka kati yao kwa njia ya kuumega mkate, ndivyo ilivyo muhimu pia kwa Wakristo kuweza kuamsha tena dhamiri zao kwa ajili ya kuambata majadiliano ya kiekumene, ili kuweza kufikia umoja kamili wa Kanisa la Kristo. Kumbe, umoja wa Wakristo ni zawadi kutoka kwa Kristo Yesu, mwaliko kwa Wakristo kujielekeza na kuwa tayari kuipokea zawadi hii katika maisha yao.

Uekumene unafumbatwa katika maisha ya sala ndiyo maana tangu mwanzo kabisa, kumekuwepo na Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo, linalohitimishwa kwa Sherehe ya Kuongoka kwa Mtakatifu Paulo, mwalimu na mtume wa mataifa. Baba Mtakatifu Francisko anasema, huu ni Uekumene wa Sala unaoendelea kuwa ni kipaumbele cha pekee katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene.

Kardinali Kurt Koch katika tafakari yake kuhusiana na mambo makuu matano yanayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene miongoni mwa Wakristo anasema ziwe ni jitihada zao za kukutana na Yesu Kristo Mfufuka, tayari kujibidisha kwenda sehemu mbali mbali za dunia kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu unaoponya na kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti! Huu unapaswa kuwa ni ushuhuda wenye mvuto na mashiko; ushuhuda wa tunu msingi za maisha ya Kikristo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.