2017-01-23 13:55:00

Pallio takatifu watakazovikwa Maaskofu wakuu kwa Mwaka 2017


Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 21 Januari anaadhimisha kumbu kumbu ya Mtakatifu Agnes, Bikira na shahidi, aliyeuwawa kunako karne ya tatu; akaonesha upendo wa pekee sana kwa Kristo mchumba wake wa daima kiasi cha kuyasadaka maisha yake ili asiuchafue ubikira wake. Yesu mwenyewe alitambulishwa na Yohane Mbatizaji kama Mwana Kondoo wa Mungu anayebeba na kuondoa dhambi za ulimwengu. Ni Mapokeo ya Kanisa kwamba, Siku kuu ya Mtakatifu Agnes, wanabarikiwa kondoo ambao manyoya yao yatatumika kutengenezea Pallio Takatifu, wanazovishwa Maaskofu wakuu katika maadhimisho ya Siku kuu ya Mtakatifu Petro na Paulo Mitume, inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 29 Juni. Baba Mtakatifu Francisko ametumia siku hii pia kubariki kondoo ambao manyoya yao yatatumika kwa ajili ua kutengenezea Pallio Takatifu watakazovishwa Maaskofu wakuu katika kipindi cha Mwaka 2017.

Pallio Takatifu ni kitambaa cha sufi safi kinachovaliwa na Baba Mtakatifu pamoja na Maaskofu wakuu wa majimbo ya Kanisa Katoliki. Hii ni alama ya Kristo mchungaji mwema; Kristo Yesu aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Ni alama ya umoja na mshikamano kati ya Maaskofu wakuu pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baada ya mabadiliko yaliyotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko, Maaskofu wakuu wapya wanavishwa Pallio Takatifu na Mabalozi wa Vatican majimboni mwao, ili kuwashirikisha waamini wengi katika tukio hili muhimu katika maisha na utume wa Kanisa mahalia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.