2017-01-23 11:41:00

Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kutimua vumbi Jan. 22 - 27, 2019


Kanisa linaendelea kujiimarisha katika mchakato wa utume wake miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, ili kuwajengea uwezo wa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa kwa njia ya utume wa vijana katika: Parokia, Majimbo, Kitaifa na Kikanda pamoja na maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani. Hili ni tukio ambalo linawakusanya vijana kutoka pande mbali mbali za dunia ili kusali, kutafakari na kufurahia zawadi ya maisha ya ujana huku wakijitahidi kumzunguka Kristo Yesu, anayepaswa kuwa ni dira na mwongozo wa maisha yao!

Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 huko Panama, yataanza kutimua vumbi kuanzia tarehe 22 – 27 Januari 2019, kwa kuongozwa na kauli mbiu “ Mimi ni mtumishi wa Bwana nitendewe kama ulivyonena” Lk. 1:38. Haya yamesemwa na Askofu mkuu Josè Domingo Ulloa Mendieta wakati akizungumza na vyombo vya habari, tarehe 20 Januari 2017. Tarehe hizi zimechaguliwa kwa kuzingatia hali ya hewa, ingawa katika baadhi ya nchi hiki si kipindi cha likizo, lakini ni matumaini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Panama kwamba, uamuzi huu hautakuwa ni kikwazo kwa vijana wengi kuweza kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, ili kukutana na Kristo Yesu, huku wakiongozwa na Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa, chini ya usimamizi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro!

Tarehe 22 hadi 27 Januari ni kipindi kizuri kinachoweza kutoa nafasi kwa vijana kuadhimisha Siku ya Vijana Duniani kwa raha zao wenyewe! Vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanakumbushwa kwamba wao ndio wahusika wakuu wa maadhimisho haya na kamwe wasiwe ni watazamaji, bali washuke huko mitini, tayari kushirikisha karama, matatizo na changamoto wanazokabiliana nazo katika maisha, kwani Kanisa linataka kuwasikiliza na kuwapatia majibu muafaka mintarafu mwanga wa Injili.

Vijana wanapojiwekea malengo mintarafu imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, mara nyingi wanajikita katika kipaji cha ugunduzi, ari, moyo mkuu pamoja na ujasiri wa kuhakikisha kwamba, malengo waliyojiwekea yanafikiwa kama yalivyopangwa. Familia ya Mungu nchini Panama inawasubiri kwa mikono miwili ili kuweza kushirikiana na kuonjesha tone la imani inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake, ili kweli vijana waweze kujisikia kuwa ni sehemu muhimu sana ya maisha na utume wa Kanisa na kamwe si “watazamaji” au “watu wa kuja”!

Vijana kutoka pande mbali mbali za dunia watashirikisha utajiri wao wa imani, mila na tamaduni njema katika maadhimisho ya Siku kuu hii ya maisha ya kiroho miongoni mwa vijana wa kizazi kipya! Itakuwa ni nafasi ya pekee kwa vijana kuweza kushuhudia uso wa ujana wa Kanisa kwa walimwengu; Kanisa linalotoka tayari kutangaza na kushuhudia Furaha ya Injili, kwa wale walioko pembezoni mwa jamii, waliotengwa au kujitenga na Kanisa kutokana na sababu mbali mbali; Kanisa linataka kwenda pembezoni mwa jamii ili kujikita katika mambo msingi ya maisha ya binadamu! Askofu mkuu Josè Domingo Ulloa Mendieta kutoka Jimbo kuu la Panama anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuanzia sasa kushiriki kikamilifu kwa hali na mali katika maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 huko Panama, Amerika ya Kusini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.