2017-01-21 17:39:00

Papa: Utume wa Wadominican umesheheni chumvi na mwanga wa Kristo!


Maadhimisho ya kilele cha Jubilei ya miaka 800 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Wadominican yaliyotanguliwa kwa Kongamano la Wadominican Kimataifa yamehitimishwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 21 Januari 2017 kwa ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano, Jimbo kuu la Roma. Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu amepembua kwa kina na mapana juu ya watu kumezwa na malimwengu kwa njia ya udadisi usiokuwa na mvuto wala mashiko na sehemu ya pili ni utukufu wa Mungu unaoshuhudiwa kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili; mambo msingi yaliyomvuta Mtakatifu Domenico na wafuasi wake, miaka 800 iliyopita kutembea katika changamoto hizi za maisha na utume wao ndani ya Kanisa!

Mtume Paulo anamtaka Mtakatifu Timotheo kuwa tayari kuhubiri Injili wakati ufaao na wakati usiofaa: karipia, kemea, na kuonya kwa uvumilivu wote na mafundisho. Hii inatokana na ukweli kwamba, watu daima wana udadisi wa kutafuta ”walimu wapya” “upendeleo””mafundisho na sera mpya! Huu ni ushuhuda maonesho ya udadisi wa binadamu; udadisi unaodanganya! Kutokana na ukweli huu, Paulo mtume anamfundisha Mtakatifu Timotheo kwa kutumia maneno makali akisema, karipia, kemea, onya, kuwa tayari na jitahidi kuvumilia mabaya.

Baba Mtakatifu anasema haya ni mambo yaliyotokea zaidi ya miaka elfu mbili iliyopita wakati Mitume wakitangaza na kushuhudia Injili ya Kristo kiasi cha kuonekana kana kwamba,  kwa sasa yamekuzwa na kuendelezwa zaidi na utandawazi unaosababishwa na kutopea kwa imani binafsi. Kuna kishawishi kikubwa cha binadamu kutafuta mambo mapya katika jamii ambamo ulaji wa kupindukia unajionesha kwa kuzungusha yale ya zamani kiasi cha kuonekana kana kwamba ni mambo mapya kabisa yenye kuvutia macho na “kuchoma moyo”.

Hata ukweli unachakachuliwa anasema Baba Mtakatifu, kiasi cha kumfanya mwanadamu kutembea katika Jamii inayoelea katika ombwe pasi na kuwa na mambo msingi na rejea katika maisha; huu ndio utamaduni mamboleo wa kutumia na kutupa! Lakini, Mwinjili Mathayo anakazia matendo mema yanayoshuhudia utukufu wa Mungu; mambo yanayotendwa na wafuasi wa Kristo Yesu, kiasi cha kuwa ni chumvi na mwanga wa mataifa unaong’ara na kuangaza mbele ya watu wanaomtolea Mungu utukufu. Huu ndio msingi thabiti kwa jamii inayoelea na kuogelea katika ombwe!

Wafuasi wa Kristo wanaweza kutenda mema kutokana na nguvu ya Kristo Yesu na Roho Mtakatifu anayewasaidia watu kuwa na moyo wa shukrani kwa Mwenyezi Mungu, kielelezo makini cha ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Baba Mtakatifu anasema Ole wake chumvi inayokosa ladha! Ole wake Kanisa linapokosa ladha! Ole wake Shirika, Padre au mtawa anapokosa ladha katika maisha na utume wake! Mama Kanisa anamshukuru na kumtukuza Mungu kwa kazi kubwa iliyofanywa na Mtakatifu Dominico!

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha mahubiri yake kwa kusema, huu ni utume ambao umesheheni chumvi na mwanga wa Kristo, ambao umetimiza takribani miaka 800 ya uwepo wake. Hii ni huduma ya Injili iliyotangazwa na kushuhudiwa kwa maneno na maisha; kazi ambayo kwa njia ya Roho Mtakatifu imewawezesha watu wengi kutomezwa na malimwengu, kiasi cha kusikiliza mafundisho ya kweli na kuonja ladha ya Injili, kiasi cha kugeuka na kuwa ni chumvi, mwanga na wajenzi wa matendo mema; ndugu wa kweli wanaomtukuza Mungu na kuwafundisha watu kumtukuza Mungu kwa njia ya matendo mema!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.