2017-01-20 15:45:00

Rais Horacio Jara wa Paraguay akutana na Papa mjini Vatican


Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 20 Januari 2017 amekutana na kuzungumza na Rais Horacio Manuel Cartes Jara wa Paraguay pamoja na ujumbe wake, ambao baadaye wamekutana na kuzungumza pia na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Mazungumzo kati ya Baba Mtakatifu na Rais Horacio yamefanyika katika hali ya utulivu na amani; kwa kuonesha uhusiano mwema uliopo kati ya Vatican na Paraguay. Baadaye, viongozi hawa wawili wamegusia masuala yanayojikita katika maendeleo endelelevu ya binadamu; mapambano dhidi ya baa la umaskini duniani pamoja na umuhimu wa kujikita katika kukuza na kudumisha haki jamii. Katika mwelekeo huu, Baba Mtakatifu pamoja na mgeni wake wamegusia mchango unaotolewa na Kanisa Katoliki katika huduma za kijamii, hususan sekta ya elimu, afya na huduma kwa maskini na wahitaji zaidi. Baadaye, viongozi hawa wawili katika mazungumzo yao, walijielekeza zaidi katika masuala ya kikanda kwa kufanya rejea katika maendeleo ya taasisi za kidemokrasia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.