2017-01-20 16:34:00

Muziki mtakatifu kama sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kiekumene


Tangu Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI alipotembelea Monasteri ya Westminster kunako mwaka 2010, kwaya ya Kianglikan kutoka Uingereza kwa kushirikiana na kwaya  ya Kipapa ya Kikanisa cha Sistina, wakajenga utamaduni wa kuimba pamoja kama sehemu ya mchakato wa kuendeleza mchakato wa kutafuta umoja miongoni mwa Wakristo, ili kumshuhudia Kristo Yesu hata kwa njia ya muziki mtakatifu.

Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa hapo tarehe 25 Januari 2017 majira ya jioni kuadhimisha Masifu ya Jioni kama sehemu ya kufunga maadhimisho ya Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo. Tukio hili litatanguliwa na Tamasha la Muziki litakaloporosmoshwa na Kwaya ya Kianglikan kutoka Monasteri ya Westminster kwa kushirikiana na Kwaya ya Kipapa ya Kikanisa cha Sistina, Jumanne tarehe 24 Januari 2017 majira ya jioni, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo nje ya Kuta za Roma. Hii ni sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kiekumene hata katika masuala ya muziki mtakatifu, kwani anayeimba vyema huyo anasali mara mbili kama alivyowahi kusema, Mtakatifu Augustino, Askofu na mwalimu wa Kanisa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.