2017-01-20 10:21:00

Iweni mashuhuda na vyombo vya Mwanga wa Kristo duniani!


Mtaguso mkuu wa pili wa Vatican, Fumbo la Kanisa yaani “Lumen Gentium” unamtaja Kristo kama Mwanga wa Mataifa ambao unapaswa kupenyezwa duniani kote. “Kristo ni Mwanga wa Mataifa. Kwa sababu hiyo, Sinodi hii takatifu katika Roho Mtakatifu kwa shauku kubwa inanuia kuupeleka mwanga wa Kristo kwa watu wote, mwanga unaong’aa katika uso wa Kanisa kwa njia ya kuitangaza na kuishuhudia Injili kwa kila kiumbe”. Huu ndiyo utume tunaopewa sisi wana Kanisa, kwenda kuwa Mwanga na sababu ya matumaini kwa wote waishio katika giza. Hili linabaki kuwa ni jukumu la Kanisa na utambulisho wake katika jamii ya wanadamu wajibu ambao bila kudhihirishwa huififisha haiba ya Kanisa na kuipoteza kabisa nafasi yake mahsusi ya kumjenga mtu katika utu.

Masomo ya Dominika ya leo, hususani somo la kwanza na somo la Injili yanatuonesha hiyo nuru inayotuzukia kwa njia ya Kristo: “Watu wale waliokaa katika giza wameona mwanga, nao waliokaa katika nchi na uvuli wa mauti Mwanga umewazukia”. Taswira inayowekwa mbele yetu ya miji miwili ya Zabuloni na Naftali katika muktadha wa zamani za Nabii Isaya inaeleweka. Hii ni miji iliyokuwa Kaskazini karibu na mipaka na “watu wa Mataifa”. Ni miji ambayo ilionekana kijamii na kidini kuwa duni kwa sababu ya mchanganyiko fulani, yaani wakazi wake hawakuwa wayahudi kwa asilimia zote. Ni miji ambayo haikupata msukumo wowote wa kidini. Sehemu hii ya nchi ndiyo ambayo Kristo anaamua kuanzia utume wake wa kimasiha. Kristo hakutaka kuanza katika mji mtakatifu wa Yerusalemu, mji wenye sifa na hadhi kubwa kidini bali anatokea katika sehemu hii duni,anaaanzia kwa hawa ambao wapo katika giza, anaigeuza sehemu hii kuwa nuru kwa watu wote.

Mbinu hii ya Kristo inazidi kujifafanua katika uchaguzi wa mitume wake wa kwanza. Yeye hatazami wale waliobobea katika dini na wanaoheshimika katika jamii bali anawachagua wavuvi, watu ambao kijamii walikuwa wanahesabika katika ya kundi ya watu wachafu kimaadili: “Ondoka kwangu, kwa kuwa mimi ni mtu mwenye dhambi, Bwana” (Lk 5:8). Ni mwendelezo wa ufafanuzi wa utume wake, utume ambao umelenga katika kumrejeshea tena mwanadamu cheo chake. Kila mmoja ameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu, kila mmoja anayo thamani kubwa mbele yake muumba. Ni ufafanuzi kwetu kwamba hakuna aliye bora zaidi ya mwingine. Kila mmoja amepenyezewa nuru ya kimbingu na kwa nuru hiyo, haidhuru inaonekana ndogo kiasi gani, Mungu ananuia kuiangazia dunia yote.

Kristo anatutaka tuwe tayari kumtumikia na katika utayari wetu anatutakasa na kututuma ili tuwe nuru yake kwa wenzetu. Dominika ya leo inatualika mimi na wewe ambao tu wabatizwa kuuwasha tena mwanga wa Kristo uliopo ndani mwetu ili tuwe mithili ya mshumaa katika chumba kilichojaa giza. Tusikate tamaa wala kuvunjwa moyo na hali zetu au hadhi zetu katika jamii. Kila mmoja katika kidogo alichonacho au kila mmoja katika hali yake hata katika udhaifu  ni chombo kiteule cha Mungu, na ni Yeye pekee anayejua namna ya kukuwezesha kuutimiza wito wake mahsusi kwako. Mwanadamu leo hii anaendelea kuishi katika hali ya kukata tamaa huku amesongwa na giza nene. Hali ya maisha katika familia, katika jamii, sehemu za kazi na penginepo haitoi chembe ya matumaini hata kidogo. Hii ni ishara kwamba sisi tunaopaswa kuwa mwanga wa Kristo tumezembea kuutimiza huo wajibu wetu.

Mara nyingi tunashindwa kuutimiza huo wajibu wetu kwa sababu hatumtangazi Yeye aliye Mwanga wa mataifa bali tunajitangaza sisi wenyewe. Wengi wetu tunajidai kutaka kutetea haki au kurekebisha mambo katika jamii lakini mara zote huwa ni kwa ajili ya faida binafsi. Swali linalotawala nafsi zetu mara zote ni: “mimi nitapata nini hapa”. Miito mingi inaitikiwa si kwa nia ya kumtangaza Kristo aliye nuru ya mataifa bali kutafuta maslahi na kukuza jina binafsi. Hatupo tayari  kutenda katika ukweli na mbaya zaidi tupo tayari hata kupindisha au kuufumbia macho ukweli ili kufanikisha malengo ya ubinafsi wetu. Rushwa, ubadhirifu wa mali za umma, kutokuwajibika na uzembe katika majukumu yetu mbalimbali ni zao la hao wanatanguliza maslahi yao mbele. Wanasahau kuwa sehemu ya madaraka waliyo nayo wamekasimiwa kwa ajili ya kuutangaza ukweli ulio nuru na jawabu sahihi kwa mwanadamu anayehangaika kuutafuta ukweli. Matokeo yake ni kuzidisha giza katika maisha ya watu.

“Akawaambia, Nifuateni, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu”. Eneo la Kapernaumu ambalo lipo katika pwani ya Ziwa Genezareti hutegemea samaki kama chakula chao muhimu. Hivyo wavuvi walikuwa ni sababu ya uhai na nguvu kwa jamii nzima kwani kazi yao iliwahakikishia shibe ya kila siku. Kristo anawaalika wamfuate kwa ajili ya kuwarudishia tena watu uhai lakini si uhai wa kimwili bali ni uhai wa kiroho uliofifishwa na giza la dhambi. Wanaitwa ili wafanywe wavuvi, yaani waundwe na kuwa na uwezo huo na kisha kwenda kutumikia na kuwaangazia watu mwanga wa Kristo. Kufanyika mitume wake kunatudai kuziacha shughuli zetu za kawaida: “Mara wakaziacha nyavu zao wakamfuata” na pia kujinasua katika mali za kiulimwengu na uhusiano wa kindugu na kifamilia: “Mara wakakiacha chombo na baba yao, wakamfuata”. Mara nyingi tunapoambatanisha mambo hayo ya kifamilia na shughuli na mali za kiulimwengu tunaingia katika kishawishi cha kujitafuta sisi wenyewe na jina letu na mwishoni ni kuubatilisha Msalaba wa Kristo.

Tunatumwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo “wala si kwa hekima ya maneno msalaba wa Kristo usije ukabatilika”. Hapa tunakiona kikwazo kikubwa sana katika kuitikia wito wetu kila mmoja kwa nafasi yake, kikwazo ambacho kwacho hutuweka katika kishawishi cha kujing’arisha sisi na nafsi zetu, hutuinua sisi tuonekane na si Kristo na Msalaba wake. Yohane Mbatizaji anatupatia mfano anaposema: “Aliye naye bibi arusi ndiye bwana arusi; lakini rafiki yake bwana arusi, yeye anayesimama na kumsikia, aifurahia sana sauti yake bwana arusi. Basi hii furaha yangu imetimia. Yeye hana budi kuzidi, bali mimi kupungua” (Yoh 3:29 – 30).

Tabia hii ni sababu ya migawanyiko isiyo ndani ya Kanisa. Migawanyiko hiyo imesababishwa na ushabiki na ubishi wa makusudi kabisa kati ya wasomi na waliobobea katika teolojia ndani ya Kanisa. Kila mmoja katika nafasi yake alikomaza mgongo wake mithili ya gumegume na kujiona yu bora katika hekima na hivyo asiposikilizwa anajing’atua na kuanzisha kundi lake. Yote haya ni makwazo na matendo yanayoubatilisha msalaba wa Kristo, fumbo ambalo linatupatia kwa muhtasari ujumbe wote wa Injili, yaani kusema ndiyo katika mapenzi ya Mungu ya kuyashika. Katika juma hili Kanisa zima linaungana na madhehebu mengine katika wiki ya kuombea umoja wa Wakristo. Tuliombee Kanisa lote na sisi wanakanisa kusudi tuweze kung’amua kasoro zetu zinazoubatilisha msalaba wa Kristo, tuzirekebishe na kuendelea kujenga kundi linaloangazwa na nuru ya Msalaba wake pekee.

Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.